bayyinaat

Published time: 26 ,February ,2018      19:25:28
News ID: 244
Masjidul Aqswa ndicho kibla cha kwanza cha Waislamu. Kwa miaka kadhaa Waislamu waliswali kuelekea Masjidul Aqswa. Katika mwaka wa pili wa Hijria, Mwenyezi Mungu alitoa amri kwa Waislamu kubadilisha kibla chao kutoka Masjidul Aqswa mjini Baytul-Muqaddas na kuelekea Masjidul Haram katika mji wa Makka. Aya za 142 hadi 150 katika Suratul Baqara zimezungumza kuhusu tukio hili. Katika sehemu moja ya aya ya 150 Mwenyezi Mungu anamhutubu Mtume SAW na Waumini kwa kusema: 

وَمِنْ حَيْثُ خَرَجْتَ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّواْ وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ لِئَلاَّ يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَيْكُمْ حُجَّةٌ إِلاَّ الَّذِينَ ظَلَمُواْ مِنْهُمْ فَلاَ تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِي وَلأُتِمَّ نِعْمَتِي عَلَيْكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ
Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na popote mlipo elekezeni nyuso zenu upande huo ili watu wasiwe na hoja juu yenu, isipokuwa wale walio dhulumu miongoni mwao Basi msiwaogope wao, lakini niogopeni Mimi - na ili nikutimizieni neema yangu, na ili mpate kuongoka.

TUKIO LA ISRAA NA MI’IRAJ.

Umuhimu wa pili wa Masjidul Aqswa miongoni mwa Waislamu unatokana na kuwa Mtume Muhammad SAW alipaa kutoka hapo na kuelekea mbinguni katika tukio la Miiraji.  Wapenzi wasikilizaji Miiraji ya Mtume SAW ilianzia Masjidul Haram mjini Makkah hadi Masjidul Aqswa ambayo inapatikana huko Baytul Muqaddas. Hapana shaka yoyote kuwa katika safari hiyo mji wa Quds ulipewa umuhimu maalumu na Mwenyezi Mungu la  sivyo Miiraji ya Mtume wa Uislamu SAW ingeanzia huko huko Makka na kwenda moja kwa moja mbinguni bila ya kupitia Baitul Muqaddas uliko msikiti wa al Aqsa.
Kuanza safari ya kimiujiza ya Mtume wa Mwisho SAW kutoka Masjidul Haram hadi Masjidul Al Aqsa ni suala linalobainisha wazi uhakika usiopingika kuwa misikiti hii miwili iko pamoja katika utakatifu.
Aya ya kwanza ya Suratul Israa ya Qur'ani Tukufu imeashiria safari hii ya kimiujiza kama ifuatavyo:
سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَى بِعَبْدِهِ لَيْلاً مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ
SUBHANA, Ametakasika aliyemchukua mja Wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara Zetu. Hakika Yeye (Mwenyezi Mungu) ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Marhum Allamah Tabatabai mwandishi wa Tafsiri ya Qur'ani ya al Mizan yenye thamani kubwa,  katika kubainisha namna Msikiti wa al Aqswa na maeneo ya pembeni mwake yalivyojaa baraka anaandika: "Ibara ya 'baarakna haulahu' yaani  tumevibariki vilivyouzunguka  ina maana kwamba, mbali na kuwa Masjidul Aqswa uko katika eneo takatifu, maeneo ya pembizoni mwake nayo ni yenye baraka. Hii ni kwa sababu eneo la pembizoni mwa Baitul Muqaddas ni la kijani kibichi na lenye rotuba likiwa limejaa miti  iliyo na matunda mengi na maji yanayotiririka na hivyo kuzidisha umaridadi wa eneo hilo. Aidha aya hiyo yamkini imeashiria baraka za kimaanawi za eneo hilo. Hii ni kwa sababu katika historia yake, ardhi ya Quds imekuwa kituo cha Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu na kitovu cha Tauhidi na ucha Mungu."
Sayyed Qutb, mfasiri wa Qur'ani kutoka Misri anaandika hivi: Israa na Miiraj inaziunganisha dini zote za tauhidi kutoka zama za Ibrahim na Ismail AS hadi Mtume wa Mwisho SAW ....Inaonekana kuwa Mtume Muhammad SAW katika safari yake ya usiku alitangaza kwamba ujumbe wake unajumuisha risala za Mitume waliotangulia na utaendeleza risala hizo."
Katika historia ya Uislamu tunasoma kuwa Mtume SAW katika tukio la Miiraj aliswali katika maeneo mbalimbali kama vile Mlima Sinai sehemu ambayo Mwenyezi Mungu alizungumza na Nabii Musa AS na vile vile Baitul Lahm sehemu aliyozaliwa Nabii Issa AS. Baada ya hapo aliingia katika Masjidul Aqswa na baada ya kusali katika mihrabu ya Mitume watukufu, alipaa na kuelekea mbinguni. Hii ndio sababu Masjidul Aqsa ukawa msikiti wenye umuhimu mkubwa sana kwa Waislamu wote.

Itaendelea….

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: