bayyinaat

Published time: 28 ,February ,2018      18:15:45
News ID: 248
Karibu mpenzi msomaji katika sehemu hii ya tatu na ya mwisho ya Makala hii ya Ijue Baytul-Muqaddas.
Tunapotazama historia ya Baytul-Muqaddas tunaona kuwa, mji huo na maeneo yake matakatifu ipo siku yatakombolewa kutoka kwenye makucha ya Wazayuni na waungaji mkono wao licha ya majeraha yote yaliyousibu. Quds na Baytul Muqaddas ni kituo kikuu na kitovu cha dini tatu za Mwenyezi Mungu yaani Uislamu, Ukristo na Uyahudi na ina nafasi makhsusi baina ya wafuasi wa dini hizo. Mji huo wa kihistoria una historia ya maelfu kadhaa ya miaka na umeendelea kusimama kidete mithili na miamba inayouzunguka. 
Jina la mji wa Byitul Muqaddas siku zote linaandamana na Quds, utukufu na utakatifu na tangu zamani mji huo wa kale ulikuwa ukijulikana kama mji wa amani na usalama. Mji huo ulikuwa eneo la Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu na majengo ya kale yaliyobakia hadi hii leo ya mji huo ni kielelezo cha historia na utambulisho wake. Makanisa ya kihistoria yaliyobakia hadi hii leo ya mji huo kama Kanisa la Ufufuo (Church of the Resurrection), misikiti ya kale hususan Msikiti wa al Aqswa ni nyaraka za historia na utambulisho wa mji wa Quds. Mji huo wa Quds pia ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu. Waislamu walikuwa wakiswali kuelekea Baytul Muqaddas hadi mwaka mmoja baada ya Hijra na kuhama kwa Mtume Muhammad (saw) kutoka Makka na kwenda Madina kwa amri yake Mwenyezi Mungu.
Kutokana na nafasi maalumu ya kidini ya mji huo mtakatifu na umuhimu wake katika dini ya Uislamu, daima Waislamu wamekuwa wakiupa heshima maalumu na nafasi ya tatu kwa utukufu baada ya miji ya Makka na Madina. 
Mwaka wa 15 Hijria (636) jeshi la Waislamu lilielekea Baytul Muqaddas baada ya kukomboa Sham. Jeshi hilo liliuzingira mji huo kwa kipindi cha miezi minne na kukabiliana na mashaka makubwa hadi lilipofanikiwa kuukomboa bila vita wala mauaji. Watawala wa Baytul Muqaddas ambao walikuwa wamepoteza matumaini ya msaada wa Warumi na wakazi wake ambao walikuwa wamechoshwa na udhaifu na utawala mbaya wa viongozi wao, walipendekeza kwamba, mji wa Baytul Muqaddas ukabidhiwe kwa Khalifa na mtawala wa Waislamu. Jeshi la Waislamu pia lilikubali sharti la wakazi wa mji huo na kupeleka taarifa kwa Khalifa wakimtaka aelekee katika eneo hilo kwa ajili ya kukabidhiwa mji huo mtakatifu. Kwa ushauri wa Imam Ali bin Abi Twalib na vigogo wengine wa Madina, Khalifa na mtawala wa Waislamu wa zama hizo alielekea Baitul Muqaddas na kukutana na maaskofu na viongozi wa kidini kisha akaandika hati ya kuwadhaminia amani na usalama, na Baitul Muqaddas ikakabidhiwa kwake. Baada ya hapo Waislamu waliujenga upya mji huo mtakatifu ambao ulikuwa umeharibiwa na kufanywa magofu.   
Miongoni mwa majengo muhimu ya kidini ya mji wa Baitul Muqaddas ni Msikiti wa al Aqswa ulioko upande wa mashariki wa mji huo ukielekea kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu ya al Kaaba, kibla cha Waislamu. Msikiti huo haukuwa kama ulivyo hivi sasa kabla ya kudhihiri dini ya Uislamu. Maeneo yote ya Haram ikiwemo Qubbatu Sakhrah (قبةالصخرة) (The Dome of the Rock) yalihesabiwa kuwa sehemu ya Msikiti wa al Aqsa. Hata hivyo hii leo msikiti mkubwa uliopo kusini mwa uwanja wa Haram ndio unaopewa jina hilo. Ujenzi wa jengo jipya la Msikiti wa al Aqswa ulianzishwa mwaka 74 Hijria na mtawala Abdul Malik bin Marwan na kukamilika katika mwaka wa kwanza wa utawala Waliid bin Abdul Malik. Urefu wa msikiti huo ni mita 88 na upana wake una mita 55 na umejengwa katika ardhi yenye ukubwa wa mita 4400 za mraba. Mwandishi wa Kifaransa Gustave Le Bon ameandika katika kitabu cha The World of Islamic Civilization kwamba: "Msikiti wa al Aqsa ni miongoni mwa majengo muhimu zaidi na ya kustaajabisha yaliyojengwa na mwanadamu na umaridadi wake hautasawariki."

Abuu Haidary, [28.02.18 06:24]
Qubbatu Sakhrah (قبةالصخرة ) (The Dome of the Rock) ni miongoni mwa athari muhimu za Kiislamu za mji wa Quds (Jerusalem). Miiraji ya safari ya kelekea katika ulimwengu wa malakuti ya Mtume Muhammad (saw) ilianzia katika mwamba ulioko katika eneo hili. Jengo hilo lilijengwa na kukamilishwa mara mbili mwaka 72 na 78 Hijria katika zama za utawala wa Abdul Malik bin Marwan. The Dome of the Rock au قبةالصخرة iko umbali wa mita 500 kutoka Masjidul Aqsa. Msomi mmoja wa Ulaya anasema: "Nimeona na kushuhudia majengo mengi huko India na Ulaya lakini hadi sasa zijawahi kuona jengo maridadi na zuri kuliko Qubbatu Sakhrah." Mbali na majengo hayo mawili, kuna majengo mengine mengi ya kiutamaduni na kidini kama misikiti, madrasa na turathi za Kiislamu katika mji wa Baytul Muqaddas (Jerusalem) ambazo zinaakisi adhama, maendeleo na ustaarabu wa Waislamu katika karne zilizopita. Misikiti 36 ya kale, makaburi ya Masahaba wa Mtume Muhammad (saw) kama kaburi la Ubada ibn Al-Samit al Ansari aliyekuwa kadhi wa kwanza Mwislamu katika mji wa Baytul Muqaddas, Hospitali ya Fatimi, Qubbatul Miiraj, Darul Hadith, Darul Qur'ani na kadhalika ni miongoni mwa vielelezo muhimu vya Kiislamu vya mji wa Baytul Muqaddas (Jerusalem). 
Baytul Muqaddas (Jerusalem) ilikuwa mikononi mwa Waislamu hadi mwishoni mwa karne ya 5 Hijria. Hata hivyo utawala na usimamizi mbovu wa baadhi ya watawala Waislamu, udhaifu, kuporomoka na migawanyiko na hitilafu zilizojitokeza baina ya Waislamu viliimarisha nafasi ya maadui zao. Mwaka 490 Hijria Watu wa Msalaba (Crusaders) walikusanya jeshi kubwa katika maeneo yote ya Ulaya na kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Baitul Muqaddas. Jeshi hilo la Msalaba lilitumia njia za kikatili kupita kiasi na hatimaye likauteka na kuukalia kwa mabavu mji huo. Jeshi al Msalaba liliua Waislamu laki moja katika eneo la Haram tukufu ya Msikiti wa al Aqswa peke yake. Katika kipindi chote cha miaka 91 ya kukaliwa kwa mabavu Baytul Muqaddas na Msikiti wa al Aqsa, msikiti huo ulikaribia kuwa gofu na kuharibika kabisa hadi Kamanda Salahuddin Ayyubi alipoukomboa mji wa Akka mwaka 583 Hijria na kuelekea Baitul Muqaddas. Salahuddin Ayyubi aliukomboa mji huo mtukufu kutoka kwenye makucha ya wapiganaji wa Jeshi la Msalaba tarehe 17 Rajab mwaka 583 Hijria. Baada ya kukomboa mji huo, Ayyubi alitoa hotuba ndani ya Msikiti wa al Aqswa na akauosha kwa uturi baada ya kuukarabati na kuusafisha. Salahuddin Ayyubi pia aliweka humo minbari maridadi na nzuri kutoka Sham. 
Wassalaamu Alaykum Warahamtullahi Wabarakaatuh

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: