bayyinaat

Published time: 09 ,March ,2018      20:43:52
News ID: 256

Sheikh Rawil Gaynetdin, Mufti Mkuu wa Russia amesema kuwa, idadi ya Waislamu nchini Russia sasa imefikia watu milioni 25 kati ya watu milioni 145 nchini humo. 
Ameongeza kuwa, idadi ya Waislamu Russia inazidi kuongezeka kutokana na sababu mbili muhimu, kwanza ni ongezeko la watoto wanaozaliwa katika familia za Waislamu na pili ni wahajiri kutoka eneo la Asia ya Kati. Amesema hata katika sensa ya serikali, idadi ya Waislamu pia imebainika kuongezeka.
Sheikh Gaynetdin amesema kwamba, aghalabu ya Waislamu nchini Russia wanaishi katika mji mkuu Moscow na miji mingine mikubwa kama vile St. Petersburg and Yekaterinburg. Kadhalika kuna idadi kubwa ya Waislamu katika majimbo yaliyokuwa ya Kiislamu kabla ya kuundwa shirikisho la Russia. Maeneo hayo ni pamoja na Tatarstan, Bashkortostan na Jamhuri za Caucasus Kaskazini, amesema Mufti huyo. Jamhuri za Caucasus au Kavkazia Kaskazini ni pamoja na Adygea, Chechnya, Dagestan, Ingushetia, Kabardino-Balkaria, Karachay-Cherkessia, Krasnodar Krai na Ossetia Kaskazini. Jamhuri zote hizo ziko katika Shirikisho la Russia lakini zenye mamlaka ya ndani ya kujitawala.
Aidha Sheikh Gaynetdin amesema Waislamu ni wenyeji wa Russia ambapo zaidi ya kaumu 58 nchini humo zimekuwa za Waislamu tangu jadi.
Aidha amesema Uislamu uliwahi kutangazwa kuwa dini rasmi ya serikali katika moja ya majimbo ya Russia ya leo yaani, Volga Bulgaria, mnamo mwaka 922, miaka 66 kabla ya Ukristo wa Kiothodoxi kukubaliwa kama dini rasmi ya serikali katika utawala wa Kievan Rus.
"Uislamu uliingia Russia katika karne ya saba Miladia. Wafuasi wa Mtume Muhammad SAW waliwasili Russia miaka 22 baada ya mtukufu huyo kuaga dunia. Walikuja katika mji ambao sasa unajulikana kama Derbent, kusini mwa Daghestan. Adhana ya kwanza Russia ilikuwa katika ardhi ya Daghestan," amebainisha Mufti.
Aghalabu ya Waislamu wa Russia wanafuata madhehebu ya Hanafi lakini pia kuna Masunni wa Madhehebu ya Shafi na pia kuna Mashia, ameongeza Sheikh Gaynetdin.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: