bayyinaat

Published time: 27 ,March ,2018      20:21:55
Angalia malaika, utakuta kwamba yeye ameumbwa katika mfumo wa kwamba hana kitu kikubwa zaidi ya akili ya kutii. Mwangalie mnyama utakuta kwamba ameumbwa katika mfumo wa matamanio tu. Lakini ukirudi kwa mwanadamu utakuta kwamba kwanza amekusanya mifumo yote ambayo inapatikana kwa malaika pamoja wanyama
News ID: 279


Utangulizi

Kuna wakati ni lazima mwanadamu ajitambue kwamba yeye yupo tofauti na viumbe wengine, hapa namaanisha viumbe mfano wa malaika na wanyama. Kwa maana endapo tutatupa jicho kwa viumbe hawa tutakuta kwamba mfumo mzima wa uumbwaji wao unatofautiana na mfumo mzima wa uumbwaji wa binadamu.

Angalia malaika, utakuta kwamba yeye ameumbwa katika mfumo wa kwamba hana kitu kikubwa zaidi ya akili ya kutii. Mwangalie mnyama utakuta kwamba ameumbwa katika mfumo wa matamanio tu. Lakini ukirudi kwa mwanadamu utakuta kwamba kwanza amekusanya mifumo yote ambayo inapatikana kwa malaika pamoja wanyama, kwa maana mwanadamu ana akili ya kutii (Mfano wa malaika) kama ambavyo pia ana matamanio (mfano wa wanyama), kisha mbali na hayo unakuta mwanadamu ana kitu cha ziada ambacho nitapenda tukiite akili ya kupambanua.

Na kitu hiki cha tatu huwezi kukikuta kwa malaika wala mnyama wa aina yeyote ile, na ndio maana Mwenyezi Mungu baada ya kuumba mwanadamu akasema kwamba amemuumba katika umbile lililokamilika zaidi.

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ

"......Bila ya shaka tumemuumba mwanadamu kwa umbile lililo bora kabisa”.[1]

Kama ambavyo pia utakuta Imamu Ally bin Abi Twalib anaelezea katika maneno yake:

فمثلت إنساناً ذا أذهان يجيلها، وفكر يتصرف بها، ومعرفة يفرق بها بين الحق والباطل، معجوناً بطينة الألوان المختلفة، والأضداد المتعادية، والأخلاط المتباينة"

".....Mwanadamu ambaye ameumbika katika pande tatu, ana ubongo ambao anaendeshea mambo yake, ana fikra ambayo kwayo anatawala kila jambo, pia ana maarifa ambayo kwayo hupambanua baina ya haki na batili. Mwanadamu ambaye amepambika kwa mambo ya aina mbalimbali yenye kupingana na kukingana.....”[2]

Baada ya kuangalia maneno ya Imamu kuna jambo ambalo ni muhimu kwa kila mwanadamu kuweza kulijua na hatimaye kulifanyia kazi, nalo ni kwamba kumbe huyu mwanadamu ambaye ameumbwa kwa mkusanyiko wa nguvu tatu tofauti, bado kuna mambo mengine mengi sana ambayo anayo, na mambo haya si yenye kufanana, bali ni yenye kutofautiana kabisa, hivyo tunafikia katika natija kwamba mwanadamu ana safari ndefu mno ya kuweza kumjua mola wake.

Kwanini nasema hivi?, ni kutokana na kwamba kumjua Mwenyezi Mungu kunasimamia katika kujitambua kwanza, sasa je huyu mwanadamu taari ameshajitambua kisha ndio apande daraja ya kumtambua muumba wake?.

Usikate tamaa ewe ndugu yangu, kwani bado una afasi ya kuweza kujitambua na kuijua nafsi yako na kisha kufikia katika hatua ya kumjua muumba wako pia. Na ndio maana katika dini yetu ya Uislamu kuna kila aina ya mafundisho ambayo yamewekwa kwa lengo la kukumbushana yale ambayo yanalenga kumjuza mwanadamu nafsi yake kwanza ikiwa ni kama njia ya kuelekea katika kumjua Muumba wake.

Katika makala hii tutajaribu kuelezea baadhi ya mambo au nguvu ambazo zinapatikana kwa mwanadamu, nguvu ambazo zinaingia katika orodha ya zile nguvu nyingi alizoziashira Imamu na kusema kwamba zinapatikana katika mwili wa mwanadamu, na huwa ni zenye kupingana daima, nguvu ambazo endapo mwanadamu atazitumia vyema basi bila shaka atafika katika yale anayoyakusudia, lakini kinyume na hivyo bado itakuwa ni mtihani.

1. Nguvu ya kula na kunywa

Bila shaka kila mwanadamu anahitajia mambo mawili muhimu kwa ajili ya kuendelea kuishi, nayo ni kula pamoja na kunywa. Na mambo haya ni mambo ya kitabia ambayo Mwenyezi Mungu ameyaumba kwa mwanadamu ili tu mwanadamu huyu aendelee kuishi kwa muda na wakati wake. Hivyo kwa ibara nyepesi tunaweza kusema kwamba nguvu ya kula na kunywa ni neema kwa mwanadamu.

Lakini neema hii inaweza kubadilika na kuwa balaa, na hii ni pale ambapo mwanadamu huyu atageuza kula na kunywa kuwa ndio lengo lake asilia, badala ya kuwa kwamba ni kwa ajili tu ya kuhakikisha kwamba anabakia hai ili aweze kutimiza majukumu mengine makubwa. Na kujisahau huku ndipo tunakuta kwamba athari zake mwanadamu anasahau kabisa hata yale masharti ambayo amewekewa katika kula na kunywa kwake, kwa sababu wakati huo kunakuwa hakuna jambo zaidi ya kula na kunywa katika maisha yake.

Angalia moja ya mambo ambayo yamewekwa kama msingi wa kula na unywa kwa wanadamu, Imamu Ally (as) anasema:

"ولا تُدخلوا بطونكم لَعَق الحرام فإنكم بعين من حرّم عليكم المعصية وسهَّل لكم سبل الطاعة"

"...Jihadharini sana na kuingiza tonge la haramu katika matumbo yenu, kwani siku zote mpo katika jicho la aliyewaharamishia maasi na akawatengenezea njia ya kutii....”[3]

Kwamba katika ulaji wetu bado ni lazima tutambue kwamba Mwenyezi Mungu ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kutupangia nini tule na nini tusile anatuona. Hivyo kumbe hata katika kula na kunywa kwetu bado ni lazima Mungu awe mbele ya chakula chetu. Hii yote maana ni kwamba kula na kunywa sio lengo la wanadamu, bali ni njia ya kufikia baadhi ya mambo makubwa. Imamu Ally (as) anasema tena katika kutukumbusha:

"إن البهائم همها بطونها، وأن السباع همها العدوان على غيرها"

"......Hakika wanyama siku zote malengo yao ni matumbo yao, na baadhi yao lengo lao kubwa ni ni kushambulia wengine tu[4]

Au pale aliposema:

"فما خلقت ليشغلني أكل الطيبات كالبهيمة المربوطة همها علفها"

"...Wala sikuumbwa kwa ajili ya kushughulishwa na kula vizuri mfano wa mnyama ambaye hafikirii zaidi ya malisho yake[5]

Sasa ni juu ya mwanadamu kuweza kufikiria na kujipima mwenyewe, kwamba ni sahihi awe kama mnyama ambaye hana fikra nyingine tofauti na kula na kunywa tu, au atumie kula na kunywa kama njia yakuweza kuwa hai kwa ajili ya kufanikisha ufaulu wake wa siku ya mwisho?.



[1] Surat Tin Aya 4

[2] Nahjul Balagha hotuba ya kwanza

[3] Nahjul Balagha hotuba ya 151

[4] Nahjul Balagha, Hotuba ya 153

[5] Nahjul Balagha Kitabu cha 15 hadithi ya 45


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: