bayyinaat

Published time: 05 ,March ,2017      17:11:00
Bwana Mtume (s.a.w.w) aliulizwa na masahaba zake; ni nini hiyo akili? akawajibu; “ni kutenda jambo kwa kumtii Mwenyezi Mungu, na watendao matendo mema hao ndiyo wenye akili”.
News ID: 28



   AKILI NI NINI?

Akili ni chombo alichopewa mwanadamu ili kutofautisha kizuri na kibaya, halali na haramu, mubaha na makuruh, na kwa sababu hii mwanadamu akawa bora kuliko mnyama.

Je Mwenyezi Mungu amezungumziaje akili? Anasema " na ule mfano tumewapigia watu, na hawauelewi isipokuwa wale wenye akili” Nahl:12.

”Hivyohivyo tunazifafanua aya zetu kwa watu wenye akili” Rum;27.

"Lau tungekuwa ni wenye kusikia au wenye akili, tusingekuwa watu wa motoni” Mulk; 10.

Aya zote hizo hapo juu zinazungumzia  uzito wa akili, akili ndiyo ambayo inakuongoza katika kutenda jambo  lolote lile. mwenye akili iliyosalimika atafanya matendo mazuri na yenye kuridhisha na mwenye akili mbayo ina kasoro, atafanya matendo mabaya na yenye kuchukiza.

Bwana Mtume (s.a.w.w) aliulizwa na masahaba zake; ni nini hiyo akili? akawajibu; "ni kutenda jambo kwa kumtii Mwenyezi Mungu, na watendao matendo mema hao ndiyo wenye akili”.

Bwana Mtume( s.a.w.w) alimwambia Ali(a.s); "Ewe Ali! pindi waja wakijikurubisha kwa muumba wao kwa mema, basi wewe jikurubishe kwa muumba wako kwa akili utawashinda, hakika sisi Mitume tunazungumza na watu kwa kiasi cha akili zao”.

Kwa hivyo hapo tunaona umuhimu wapekee wa akili aliyopewa mwanadamu, pia ametakiwa aitumie akili hiyo katika kupambanua mambo kwa kutumia akili ,katika mafunzo anayotupa Bwana Mtume (s.a.w.w) kuhusu akili, anasema: "hakugawa Mwenyezi Mungu kwa waja wake kitu kilicho bora zaidi kuliko akili, usingizi wa mtu mwenye akili ni bora zaidi kuliko kukesha kwa mtu mjinga (asiye na akili)".

Na hakutumwa nabii yoyote wala mjumbe yoyote mpaka awe amekamilika kiakili, na akili yake iwe ni bora kuliko akili za watu wote, na huenda katika watu hao akawepo mtu mwenye kujitahidi zaidi lakini hawezi  kumshinda huyo Mtume”.

Hadithi hii yaonyesha kuwa mtu mwenye akili hata kulala kwake ni bora kuliko kukesha kwa mtu asiye na akili, kwani kukesha huko hakuna maana yoyote ikiwa anayoyafanya hayaendani na akili iliyosalimika, mfano hivi leo utawaona watu  wanashinda au wanakesha katika ngoma, disko, taarabu, drafti, karata n.k .na wengine wakitoa fedha nyingi kwa ajili ya mikesha hiyo je hiyo ni sawa kwa mwenye akili?

Imepokewa kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) yeye alimwambia mmoja wa masahaba wake aliyeitwa Uwaymir "Ewe Uwaymir zidisha akili, utazidi kuwa karibu na mola wako na kuwa na akili ni utajiri!! Uwaymir akasema; nakufidia baba yangu na mama yangu, nifanye nini kwa hiyo akili?  Bwana Mtume (s.a.w.w) akasema "jiepushe na haramu za Mwenyezi Mungu, na tekeleza faradhi za mwenyezi mungu utakuwa ni mwenye akili! Kisha tenda matendo yaliyo mema utawazidi waliyopo duniani kwa akili, na utazidi kuwa karibu kwa mola wako kwa utukufu”

VIPI TUTAHIFADHI AKILI ZETU ILI ZIBAKIE SALAMA?

Tunahimizwa tujiepushe na mambo ya haramu yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu, na tutekeleze ibada zetu kwa amri ya mwenyezi mungu ndipo utakuwa mwenye akili, hapa tunamuomba  msomaji wetu awe makini kuelewa kinacho kusudiwa. Tunapozungumzia akili na mtu mwenye akili, na kusema kwamba fulani ana akili na fulani hana akili, tunakusudia utendaji kazi wa akili ya kila mtu, kwani akili ni kifaa ambacho kila mtu amepewa na Mwenyezi Mungu, kama hadithi inavyosema:

أخبرنا أبوجعفر محمد بن يعقوب قال: حدثني عدة من أصحابنا منهم محمد بن يحيى العطار عن أحمد بن محمد، عن الحسن بن محبوب، عن العلاء بن رزين، عن محمد بن مسلم، عن أبي جعفر عليه السلام قال: لما خلق الله العقل استنطقه ثم قال له: أقبل فأقبل ثم قال له: أدبر فأدبر ثم قال: وعزتي وجلالي ما خلقت خلقا هو أحب إليّ منك ولا أكملتك إلا فيمن احب، أما إني إياك آمر، وإياك أنهى وإياك اعاقب، وإياك اثيب

Wapokezi wa hadithi hii wanaishia kwa Abu Jafari ambaye ni Imam Baqir anasema: pindi Mwenyezi Mungu alipoiumba akili, alizungumza nayo, kisha akaiambia nenda mbele ikaenda ,kisha akaiambia rudi nyuma ikarudi, na hapo Mwenyezi Mungu akasema, kwa nguvu zangu na utukufu wangu sikuumba kiumbe ambaye nampenda sana kuliko wewe na wala sikukuumba na kukukamilisha isipokuwa ni kwa yale ninayoyapenda, ama kwako nitaamrisha ,na kwako nitakataza, na kwako nitaadhibu, na kwako nitatoa thawabu.

Na kifaa hiki Mwenyezi Mungu akakiweka ndani ya kila mwanadamu ili kifanye kazi na sasa tukiwa tunajibu swali letu la vipi tutahifadhi akili ili ibakie salama, na ibaki inafanya kazi, tunamaanisha kwamba kuna baadhi ya matendo, ambayo mwanadamu anayafanya ambayo yanapelekea kudhoofika nguvu ya akili au kupotea kabisa, hapa ndipo tutasema fulani akili yake haiko sawa au fulani hana akili. na wakati mwingine tunazungumzia akili tukiwa tunakusudia elimu, na tunafanya hivyo kwa sababu makazi ya elimu ni ndani ya akili, kwa hiyo tukisema kwamba kuna mambo yakifanywa yatadhoofisha akili, iwe akili kwa maana ya akili ya asili itadhoofika, au iwe akili ambayo ni elimu na ambaye inakaa ndani ya akili kama akili yenyewe, vyote vitadhoofika. (yaani akili na elimu inayokaa ndani ya akili, ambayo wakati mwingine inaitwa akili, na hii ndiyo akili iliyokamilika).

Mtume (s.a.w.w) anasema :akili ina vigawanyo vitatu, ambaye atakuwa navyo akili yake imekamilika na ambaye hana vigawanyo vivyo hana akili.1-kuwa na maarifa sahihi juu ya Mwenyezi Mungu,2-kumtii inavyotakiwa,3-na kuwa na subira isiokatika juu ya yale anayoyaamrisha, tukitimiza haya akili zetu zitabakia salama.         

 وقال نبي الرحمة (ص) إذا أذنب العبد ذنبا فارقه عقل لا يعود إليه أبدا

Mtume (s.a.w.w) anasema atakapofanya mja dhambi akili inajitenga naye na hairudi abadani.

Bwana Mtume (s.a.w.w) amesema; "kichwa chenye akili baada ya imani na Mwenyezi Mungu kinapendana na watu” na kupendana na watu ni dalili ya kuwa na akili nzuri na timamu.

 

 

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: