bayyinaat

Published time: 02 ,April ,2018      20:56:22
Lakini la kushangaza kwa sasa, watu ambao wanajiita Waislamu tena kwa kudai kuwa wao ni Waislamu bora na safi (na hatuna haja ya kukitaja jina kwani ni maarufu kwa kujinadi kuwa wao ndiyo Waislamu safi na wasiokuwa wao ni makafiri),
News ID: 288

kwa mtazamo wa Uislamu, hakuna anayepinga kwamba kimaumbile ya asili ya mwanadamu anapenda amani, ama fujo na ghasia ni mambo ambayo yako nje ya maumbile ya mwanadamu, na Uislamu siku zote unapenda kuendeleza amani ya mwanadamu, hata kama atakuwa sio Mwislamu, labda kama atauletea Uislamu matatizo, hapo dini ya Kiislam haiwezi kamwe kudhamini amani yake, bali kinyume na hapo, Uislamu utaamrisha jihadi dhidi yake.

Lakini la kushangaza kwa sasa, watu ambao wanajiita Waislamu tena kwa kudai kuwa wao ni Waislamu bora na safi (na hatuna haja ya kukitaja jina kwani ni maarufu kwa kujinadi kuwa wao ndiyo Waislamu safi na wasiokuwa wao ni makafiri), ambao hutumia dini vibaya, na kwa sasa, dini ya kiislam inaonekana kama dini ya fujo, kawaida hakuna jihadi baina ya Waislamu kwa Waislamu, Mtume hakuiasisi wala Mwenyezi mungu, bali jihadi ni baina ya Waislamu na makafiri ambao wanaupiga Uislamu waziwazi au kisirisiri. lakini kikundi hiki ambacho kimepotoka chenyewe kilianzisha vurugu na fujo baina ya Waislamu kwa ajili ya kutimiza matakwa ya nchi za magharibi, na kuyaita matendo yao kuwa ni jihadi. na Allah atukinge na fikira hizi chafu.

ALLAH KATUWEKEA MISINGI YA KULINGANIA WATU, IMA WAWE NI WAISLAMU AU SIO WAISLAMU

Mfano:

Mwenyezi Mungu anatufundisha ni vipi tutawalingania, wale ambao sio Waislamu, na wale ambao ni waovu katika Waislamu, anasema: na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu na hao ndio walio fanikiwa. suratul-imran 104. Na sehemu nyingine anasema:

Waite waelekee kwenye njia ya mola wako mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. mola wako ndiye anaye mjua zaidi aliyepotea njia yake, na yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongaka.

Kwa hiyo njia zote za ufikishaji, Mwenyezi Mungu amezibainisha, na tunaweza kutoa maelezo mafupi kuhusu aya hizi, kwanza: Allah anataka, lipatikane kundi lenye kulingania mema na kukataza maovu, ni sharti kundi hilo liwe linafahamu mema na maovu ni yapi, kundi hili liwe linafahamu hekima, na kuitumia. ukiangalia vigezo vinavyotakiwa kwa mlinganiaji, haya makundi yanayojiita kuwa ndiyo Waislamu bora hayatimizi, utawaona wakitumia nguvu sana, kwa kueneza itikadi yao, na bila hekima.

na kwa wale ambao hawafahamu Uislamu watahukumu kwamba hivi ndivyo Uislamu ulivyo. na kwa kukosa elimu na hekima vikundi hivi, hali inazidi kuwa mbaya, na dini ya Kiislamu inazidi kuchukiwa, kwa sababu ya uovu wa watu wachache wajiitao Waislamu. mtu mmoja wa huko Marekani katika jimbo la California alichukuwa kinyesi na kuandika katika baadhi ya kuta za msikiti wa mjini humo kwamba, hii ni nyumba ya wauaji. na bila shaka hii ndio sura inayotolewa na vikundi ambavyo vinajiona kuwa wao ndio Waislamu, pamoja na kutoa fat’wa za uchochezi na ambazo zinaleta fujo na utengano katika jamii.

Mtume (s.a.w.w) anasema mwenye kufanya mambo bila kuwa na elimu nayo, anayo yaharibu ni mengi kuliko yale anayo yatengeneza.

VITA VYA KHAYBAR

Na tukiwa katika mada ya amani na fujo itabidi tuzungumzie kidogo vita vya khaybar, kwani ni katika vita kali ambavyo Waislamu walipigana, ili kuondosha fujo za Wayahudi ambao walikuwa wanaishi sehemu za Khaybar, na vita vya Khaybar ni katika vita ambavyo vilileta utukufu kwa Waislamu, na kumpandisha cheo Ali Bin Abitwalib.

Kabla ya vita vya khandaqi, Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliwatoa makabila mawili ya Kiyahudi ya banii Nadhir na banii Qaynuqaa kutoka katika mji wa Madina. makabila haya mawili yalipanga njama za kumuua Mtume (s.a.w.w).kwa kutolewa Madina kuliongezea chuki, uadui na hasadi yao dhidi ya Waislamu.walipotolewa Madina walihamia katika kijiji cha Khaybar, ambacho ni kama km 100 kutoka katika mji wa Madina. Khaybar maana yake ni mji ulozungushwa kwa ngome kubwa, ulikuwa ni mji mkuu wa Wayahudi, na walijenga hapo ngome kubwa saba, za kujikinga na kujihifadhi nazo, kutokana na shari na uadui wa yoyote atakaye wafuata huko kwa vita. na kila ngome ilikuwa na jina, na kubwa kuliko zote iliitwa Qamusi. na makabila haya siku zote yalikuwa yakifanya fitina na kuchochea fujo, na kuhamasisha makabila mengine ya kiyahudi kuwa dhidi ya Mtume na Waislamu kwa ujumla.

Na katika mwezi wa Rajabu 24 mwaka wa 7, Mtume s.a.w.w aliandaa jeshi la watu 1400, na kwa mda wa siku saba waliweza kuzifungua ngome zote.siku hizo, Mtume Muhammad (s.a.w.w) mara nyingi sana akiumwa na kichwa kikali sana mpaka hufikia mda bendera inachukuliwa na watu wengine kwenda katika mapambano.ilichukuliwa bendera na baadhi ya maswahaba wakubwa, na wote hawa hawakuweza kurudi na ushindi. mpaka ikafika wakati Mtume akasema maneno yafuatayo baada ya kuona kwamba vita hiyo inachukua muda mrefu na ushindi haujapatikana: inshallah kesho mimi nitampa mtu bendera ambaye anampenda Allah na Mtume wake, na Allah na Mtume wake wanampenda mtu huyo, ni mwenye kuthibiti na wala hakimbii vitani.

kesho yake masahaba walikuwa wanasubiri ni nani ambaye atapewa bendera na Mtume, na hapo kila mmoja alikuwa anatamani sana apewe yeye, na wakati Mtume anakagua jeshi lake, hakumuona Ali bin Abiitwalib, akauliza yuko wapi Ali a.s wakasema anaumwa, akaomba wamwite na alipokuja Bwana Mtume akamkabidhi bendera, na akamwambia nenda kafungue Khaybar. Imam Ali a.s alipigana vikali na makamanda wa Kiyahudi ambao walikuwa na uwezo mkubwa lakini aliwapiga vikali sana na kuwashinda, na mwisho alipigana na aliyekuwa kamanda wao mkuu, aliejulikana kwa jina la Mar’haba Ibun Judah na alimpiga dharuba moja ya upanga wake wa Dhul-fiqaar na kumpasua vipande viwili, na akapiga ukelele wa takbira, kama ilivyokuwa ada yake kila anapomuua adui yake vitani. katika vita hivi Wayahudi waliuliwa watu wao wapatao 93 na Waislamu walikosa watu 19. vita vya Khaybar vilimaliza upinzani wote wa Wayahudi juu ya Waislamu na kuwafanya sasa wakubali kuwa chini ya utawala wa dola ya Kiislamu na makao yake makuu ukiwa ni mji wa Madina, na hapo Bwana Mtume (s.a.w.w.w) aliweza kupunguza kiasi fulani vurugu na fujo walizokuwa nazo Wayahudi wa khaybar.

Na; Sheikh kadhim abbas.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: