bayyinaat

Published time: 22 ,April ,2018      20:32:02
kujitolea kwake katika njia ya Mwenyezi Mungu uliendelea hadi kwenye hamasa ya kihistoria ya ushindi wa damu dhidi ya upanga katika jangwa la Karbala. Ni jambo lisilo na shaka kwamba Bwana Mtume na Ahlul-Bayt wake ni viumbe bora kabisa.
News ID: 308

Imam Hussein AS alikuwa bado kijana mdogo wakati kilipojiri kisa cha Mubahala. Mtume Muhammad SAW aliwachukua Hassan na Hussein kwa jina la wanawe katika kisa hicho ambapo Wakristo wa Najiran walipoona watu aliofuatana nao Bwana Mtume yaani Bibi Faatimah, Ali na watoto wao wawili, waliogopa mno na hawakuthubutu kuendelea na upinzani wao. Kisa cha Mubahala ni maarufu kwa wanaofuatilia matukio ya Kiislamu. Lakini miaka ya furaha haikurefuka kwani ilikuwa ni takriban baada ya miaka sita ya tangu kuzaliwa Imam Husain AS ndipo alipofariki dunia Bwana Mtume SAW. Bwana Mtume ameusia sana juu ya umuhimu wa kuwapenda na kushikamana na Ahlul Bayt wake. Amma baada ya kufariki dunia Mtume na kupita miaka mingi hadi Waislamu walipomshikilia Imam Ali AS achukue uongozi wa dola ya Kiislamu, miaka yote hiyo Imam Hussein na kaka yake Imam Hassan walikuwa bega kwa bega na baba yao Imam Ali na walishiriki vilivyo katika masuala yote ya kisiasa, kijeshi na mengineyo mengi. Hata baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ali AS, Imam Hussein alikuwa bega kwa bega na kaka yake Imam Hassan katika njia ya kutangaza na kupigania dini ya Mwenyezi Mungu. Ushujaa wa Imam Hussein na kujitolea kwake katika njia ya Mwenyezi Mungu uliendelea hadi kwenye hamasa ya kihistoria ya ushindi wa damu dhidi ya upanga katika jangwa la Karbala. Ni jambo lisilo na shaka kwamba Bwana Mtume na Ahlul-Bayt wake ni viumbe bora kabisa.

Maisha ya Imam Hussein AS

Sira, mwenenendo na maisha ya Imam Hussein AS yalijaa mapenzi kwa watu. Sifa ya mtukufu huyo ya kuwa pamoja na watu wakati wote kwa shida na raha na miongoni mwa sifa za kipekee za Imam Hussein ilikuwa ni usamehevu. Kusamehe na kujitolea ni miongoni mwa sifa tukufu za waja wema. Bwana mmoja kutoka Sham aliyejulikana kwa jina la Isam alitembelea mji mtukufu wa Madina. Kwa bahati alionana na mtu ambaye sura yake ilijipambanua na ya watu wengine alipouliza huyo alikuwa ni nani aliambiwa na Hussein bin Ali mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Mwenyeji huyo wa Sham ambaye alikuwa amejazwa chuki zisizo na kifani dhidi ya Imam Ali AS na wanawe, aliona hiyo ndiyo fursa nzuri ya kutoa hiqdi na chuki kubwa aliyokuwa nayo moyoni. Bila woga wala kusita, alimkabili Imam Hussein AS kwa kila aina ya tusi, shutuma, fihi na uhasidi, alimradi alitoa kila uchukivu aliokuwa nao rohoni. Wakati wote huo Imam Hussein alikuwa anamwangalia tu. Alipomaliza kujifaragua kwa matusi, Isam alisubiri kijeuri kuona radiamali ya Imam Hussein AS. Lakini tofauti na alivyotarajia, radiamali ya Imam haikuwa ya kughadhibika wala tone la kukasirika. Alimwangalia kwa jicho la kumhurumia Bwana yule wa Sham na kwa upole akamwambia, unaonekana wewe ni mgeni hapa, kama una shida niko tayari kukusaidia, kama huna pa kufikia milango ya nyumba yangu iko wazi kwa ajili yako. Bumbuwazi lilitanda kwenye uso wa Isam, soni zikafunika paji lake la uso, akatafuta pa kuweka uso wake akashindwa kutokana na haya na kufedheheka. Isam anaendelea kusimulia kisa hicho akisema: Wakati huo nilitamani ardhi ipasuke nididimie ndani lakini hilo halikuwa." Kwa muda huo mchache, Isam alibadilika na kuwa miongoni mwa wafuasi watiifu kabisa wa Watu wa Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: