Mtume Muhammad (saww)
ni wa kwanza katika ambao wanatengeneza idadi ya maasumina 14
watakatifu, kama ambavyo pia yeye ni mtume wa mwisho katika mitume ya mwenyezi
mungu swt.
Jina lake ni Muhammad.
Baba yake ni Abdullahi.
Mama yake ni Amina binti Wahab.
Babu yake ni Abdul Mutalib.
Tarehe ya kuzaliwa ni 17 Rabiul awwal (mfungo sita) katika mji
mtukufu wa Makka.
Tarehe ya kufariki ni 28 Safar (mfungo tano) baada ya kuugua kwa
muda mrefu kutokana na sumu aliyopewa na mwanamke wa Kiyahudi.
Mahala alipozikwa ni mji mtukufu wa Madina.
Idadi ya watoto ni 6 watatu wakiwa wa kike na watatu wakiwa ni wa
kiume.
Mazazi yake matukufu
Ni siku ya Ijumaa ya tarehe 17 mnamo
mwaka ambao umejulikana kama mwaka wa tembo kutokana na tukio maarufu
lililotokea mwaka huo, ambapo nuru ya Mtukufu Mtume (saww) iliweza kudhihiri
katika ulimwengu huu. Na ili kuonyesha kwamba haikuwa ni jambo la kawaida ndio
maana tunaambiwa kwamba wakati wa kuzaliwa kwake kuna baadhi ya matukio ambayo
yalitokea siku ile, na baadhi ya matukio hayo ni kama:
1.
Kuanguka kwa masanamu ambayo yalikuwa yakiabudiwa kwa miaka mingi.
2.
Moto wa majusi ambao ulikuwa ukiabudiwa nao ulizimika kwa uzito wa
mazazi yake.
3.
Kuwaka kwa nuru ambayo iliangaza sehemu kubwa mno ya Arabuni.
Na matukio mengi sana ambayo
historia ya mazazi ya Mtume imeyabainisha, lakini hayo yote yakiwa ni katika
kuonyesha ishara ya kwamba mtu huyu aliyezaliwa hakuwa mtu wa kawaida bali
alikuwa na jambo mahususi lililopelekea kutokea kwa matukio haya.
Abuu talib (baba mdogo wa mtukufu
Mtume)
Huwezi kuzungumzia shahsia muhimu
katika maisha ya bwana mtume saww, bila ya kutaja shahsia hii, baba mdogo na
mlinzi mkubwa wa bwana Mtume saww, na hii ni kutokana na duru yake kubwa
aliyokuwa nayo katika kuhakikisha kwamba mtukufu Mtume hapatwi na madhara yeyote
kutoka kwa watu wa Maka. Na si tu kwamba alikuwa ni mwenye kumtetea basi, bali
alikuwa ni mtu ambaye pia mwenye imani juu ya utume wa mtukufu Mtume saww kama
ambavyo vitabu vya historia vinanukuu hivyo.
Kuhama kwake
Miongoni mwa matukio muhimu katika
maisha ya bwana mtume ni tukio zima la kuhama kwake Maka na kuelekea Madina. Na
kuhama huku bila shaka kulikuwa na sababu zilizopelekea kutokea kwake, kwani ni
lazima tutambue kwamba mnamo mwaka wa kumi, mwaka ambao mtukufu Mtume aliuita
kwamba ni mwaka wa huzuni kutokana na kuambatana kwa misiba miwili mizito,
msiba wa baba yake mdogo na msiba wa mke wake kipenzi bibi Khadija (ra), hivyo
hata wale ambao walikuwa wanashindwa kumuudhi mtukufu mtume kutokana na uhai wa
watu hawa, sasa walipata nafasi ya kuweza kumuudhi.
Hivyo Mtume akawa hana namna zaidi
ya kuhama na kwenda mji mwingine ambapo atapata hifadhi na kutoudhiwa. Ndipo alipojaribu
kwenda mji maarufu wa Taif, lakini kutokana na kutokubalika na watu wa mji ule
na si tu kutokukubalika bali hata kuudhiwa na kujeruhiwa pia, aliamua kupanga
safari ya kuhamia mji wa Madina ambapo alipata watu wa kumnusuru yeye pamoja na
masahaba zake, na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu harakati za kufikisha ujumbe
ziliweza kuendelea.