bayyinaat

Published time: 19 ,September ,2018      10:55:14
Alihudhuria Mjumbe wa Allah (s.a.w.w) kwenye kikao cha kijana aliyekaribia kukata roho na kumlakinisha shahada, lakini hakuweza kuitamka shahada hiyo, akauliza (s.a.w.w): Je! Anaye mama?
News ID: 320

بسم الله الرحمن الرحیم

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema mwenye kurehemu


KIJANA ANAYEFIKIWA NA UMAUTI NA SHIFAA YA MTUME

Alihudhuria Mjumbe wa Allah (s.a.w.w) kwenye kikao cha kijana aliyekaribia kukata roho na kumlakinisha shahada, lakini hakuweza kuitamka shahada hiyo, akauliza (s.a.w.w): Je! Anaye mama? Alikuwa mwanamke karibu nae akajibu: Ndio mimi ni mama yake, Mtume akamuuliza; Je! Umemghadhibikia? Akajibu: Ndio miaka sita sisemi naye, Mtume akamuomba kumridhia kijana wake Mama akamsamehe kwa utukufu wa Mtume (s.a.w.w), kisha kijana akatoa kalima ya tawhidi, Mtume alimuuliza kijana, Nini unaona kwa sasa? Akajibu: Ninamuona Mtu mweusi mwenye umbile la kikatili mwenye harufu mbaya, haachi kunilaani, Mtume akamfundisha maneno haya: (Mola wangu mwenye kukubali mepesi na kusamehe mengi, kubali kutoka kwangu mepesi na samehe yangu mengi).[1] Akasoma maneno yale, akasema: Kwa sasa ninamuona Mtu mweupe mwenye mandhari nzuri mno na mwenye uso wa bashasha lakini yu mwenye jambo la kuhofisha, na yuko kiasi mbali nami. Mtume (s.a.w.w) akasema: kariri maneno hayo mara ya pili akafanya hivyo kijana, kisha akasema: Yametoweka mazingira yake ya kutisha kabisa kabisa.

Alifurahi Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na akasema: Hakika Mwenyezi Mungu amemsamehe dhambi zake, na wakati huo kijana alifariki dunia.

Hadithi hii tukufu hutumika kuonyesha athari kubwa na natija ya kudharau wazazi wawili kuwa ni natija yenye hatima mbaya na adhabu na mwanadamu anakufa bila ya imani na atabakia katika adhabu milele, pamoja ya kwamba kijana amelakiniwa na Mtume (s.a.w.w), lakini hakuweza kutamka shahada hadi aliporidhiwa na Mama yake, na baada ya ridhaa ya Mama yake na kusoma maneno yale Mwenyezi Mungu ndipo akamridhia pia kwa baraka za Mjumbe wake.

DUA YA MALAIKA KWA MTENDA WEMA KWA BABA NA MAMA YAKE:

Kutoka kwa amirul muuminin (a.s): Kutendea wazazi wawili ni ibada kubwa mno.[2]

Na kutoka kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w): "Hakika Mwenyezi Mungu anao malaika wawili mmoja humnong’oneza mwingine kwa kusema: Mola wangu mlinde mtenda wema kwa utakaso wako, na mwingine anasema: Mola wangu muangamize muasi kwa wazazi wake kwa ghadhabu yako”.[3] Bila shaka kama ifahamikavyo Dua ya malaika hujibiwa haraka.

HAKI ZA WAZAZI WAWILI BAADA YA KUFA KWAO

Haki ya wazazi wawili baada ya kufariki ni hizi zifuatazo:

Kwanza: Ni wajibu juu ya watoto kutekeleza ibada zilizowapita wakati wa uhai wao mfano wa Hijja, Sala, Saumu na pia ni wajibu juu yao kulipa madeni yao.

Pili: Kufanyia kazi yale waliyoyausia.

Tatu: Wasiwasahau maisha yao, ni wajibu wao kuwaombea maghfira na rehema na kutoa sadaka kwa niaba yao, na watende amali za sunna na kupeleka thawabu zake kwao.

KUWAASI WAZAZI WAWILI BAADA YA KUFARIKI

Kutoka kwa Imam Sadiq (a.s): Hakika mja huwa mwema kwa wazazi wake wawili pindi wawapo hai kisha wanapofariki halipi madeni yao wala kuwaombea maghfira, Hakika Mwenyezi Mungu humuandika katika waja wenye kukiuka haki za wazazi, na huhesabika muasi wakati wa uhai wao, na na hakika atakayekuwa muasi kwao wakati wa uhai wao watakapofariki akalipa madeni yao basi Mwenyezi Mungu atamuandika katika waja wema…[4]

NUKTA ZA HESHIMA KWA WAZAZI

Hakika kutendea wema wazazi na kutekeleza haki zao na kulinda adabu na heshima imekuja katika hadithi mambo ambayo yametajwa katika riwaya za Ahlul bayt (a.s) na ambazo yatupasa kuzilinda, na tutaashiria baadhi hapa:

1. Endapo mmoja wenu atataka kumuita mzazi wake basi asiwanadi kwa majina yao, bali atumie lakabu na kunia zao.

2. Asiwatangulie na asikae kabla yao.

3. Asianze kula chakula kabla yao.

Imam Sajjad (a.s) hakuchangia wala kushiriki sahani moja ya chakula na mama yake, kwani alikuwa akisema; Ninaogopa kunyoosha mkono wangu kwenye tonge ambalo akilitaka mama yangu nikawa kwa jambo hili nimekhalifu adabu na kutolinda heshima ya mama.

4. Asigeuze uso wake kwao katika kikao.

5. Asipaaze sauti yake juu ya sauti zao katika maongezi.

6. Asinyanyue mkono wake juu ya mikono yao.

7. Asitende jambo ambalo litapelekea Baba na Mama yake kutukanwa na kushutumiwa, kama vile asimtukane baba wa yeyote asije kutukaniwa baba yake.

Imepokelewa kuwa Imam Sajjad (a.s) alikuwa akitembea njiani akamuona Mtoto akiegemea mkono wa baba yake, alighadhibika (a.s) kwa kitendo kile na hakumsemesha milele, hadi mwisho wa umri wake.



[1] Al- Mustadrak, juz 15, uk 189, mlango 85, hadithi 9.

[2] Al- mustadrak, juz 15, uk 178, mlango wa 68, hadithi 21.

[3] Al- mustadrak, juz 15, uk 178, mlango wa 68, hadithi 15.

[4] Usul al- Kafiy, juz 2, uk 163, mlango; al- birr bil waalidayn, hadithi 21.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: