bayyinaat

Published time: 19 ,September ,2018      11:35:26
Katika madhambi mengine makubwa ni kula mali ya yatima, kwa maana Mtoto ambaye hajabaleghe na amefariki Baba yake. Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na Maimamu watukufu Amir al- Muuminin (a.s) na Imam Kadhim na Imam Ridhaa (a.s) na Imam Jawad (a.s) wanaihesabu amali hii
News ID: 323

بسم الله الرحمن الرحیم

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema mwenye kurehemu


Katika madhambi mengine makubwa ni kula mali ya yatima, kwa maana Mtoto ambaye hajabaleghe na amefariki Baba yake.

Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na Maimamu watukufu Amir al- Muuminin (a.s) na Imam Kadhim na Imam Ridhaa (a.s) na Imam Jawad (a.s) wanaihesabu amali hii ya kula mali ya yatima ni katika madhambi makubwa mno, na zimepokelewa kemeo nyingi za adhabu ya moto katika Aya nyingi za Qur’ani aliposema Mwenyezi Mungu mtukufu:

"إِنَّ الَّذِينَ يأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيتَامَى ظُلْمًا إِنَّمَا يأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا وَسَيصْلَوْنَ سَعِيرًا".

"Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni”.[1]

Imenukuliwa kutoka katika tafsir al- kabir kwamba, siku atakayo fufuliwa mlaji wa mali ya yatima, utamtoka moto kinywani mwake, na moshi pia kinywani mwake na masikioni mwake na machoni mwake na kwenye ulimi wake wakati huo watamjua watu kuwa ni mlaji wa mali za yatima kwa alama hizi. Na sentensi hii kwamba () ni tishio la mwisho ambalo kwamba ulaji wa mali za yatima ni sababu kamili ya kuingia mtenda jambo hilo motoni na si sababu nyingineyo, kwani dhambi hii ni katika madhambi makubwa mno mbele za Mwenyezi Mungu.

Anasema Mwenyezi Mungu mtukufu:

"وَآتُوا الْيتَامَى أَمْوَالَهُمْ وَلَا تَتَبَدَّلُوا الْخَبِيثَ بِالطَّيبِ وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَهُمْ إِلَى أَمْوَالِكُمْ إِنَّهُ كَانَ حُوبًا كَبِيرًا".

"Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa”.[2] Na hapa Mwenyezi Mungu alingania watu kuacha kula mali za yatima, na hatimaye kuzikabidhi kwao wakuapo, na wala musichanganye mali ya haramu ambayo ni mali ya yatima pamoja na mali ya halali ambayo ni mali yenu. Na muhtasari wa jambo hili ni kwamba: Musinyooshe mikono yenu kwenye mali za yatima kwa kuchukua mali yake yenye thamani kwake na kuiweka mali hiyo katika mali zenu zenye thamani ndogo.

Na amesema tena (s.w.t):

"وَلْيخْشَ الَّذِينَ لَوْ تَرَكُوا مِنْ خَلْفِهِمْ ذُرِّيةً ضِعَافًا خَافُوا عَلَيهِمْ فَلْيتَّقُوا اللَّهَ وَلْيقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا".

"Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeliacha nyuma yao watoto wanyonge wangeliwakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa”.[3] Hivyo yawapaswa watu kuogopa kumdhulumu yatima na kuwa na tahadhari na matendo mfano wa hayo, ni wajibu kwao kuamiliana nao kwa muamala mwema, na yeyote amhofiaye mwanaye baada ya kufa kwake kwa kupoteza mali zake na kunyang’anywa haki yake ni juu yake kumuogopa mwenyezi Mungu katika suala mzima la yatima na amche Mungu na kujiepusha kudhulumu yatima kwani katika natija ya kuwadhulumu mayatima wa watu ni dhulma kufikia kizazi chake, na wanawe kupatwa na kile alichokitenda baba kwa mayatima.

Hakika Aya zimeweka bayana juu ya ukubwa wa dhambi hii.

KUTAKUWAPO MALIPO MFANO WAKE:

Imepokelewa kutoka kwa Imam Sadiq (a.s) kuwa amesema: Hakika Mwenyezi Mungu mtukufu amekemea vikali katika mali za yatima adhabu aina mbili ama mojawapo ni adhabu ya siku ya mwisho ambayo ni moto, na ama adhabu ya dunia ni kwa mujibu wa ile kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"وَلْيخْشَ الَّذِينَ لَوْ تَرَكُوا مِنْ خَلْفِهِمْ ذُرِّيةً ضِعَافًا خَافُوا عَلَيهِمْ فَلْيتَّقُوا اللَّهَ وَلْيقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا".

"Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeliacha nyuma yao watoto wanyonge wangeliwakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa”.”. [4]

Na katika wasia huu imekuja tahadhari ya wazi kwa wausiwao kuhusu mali ya yatima kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu katika amali zao na wasisimamie kutenda matendo ambayo yatakuta watoto wao baada ya kufariki kwao.

Kisha Aya imetaja tena kile alichokieleza Amirul muuminin (a.s) na Imam Sadiq (a.s) kuhusu maana ya kile kitakacho wasibu siku ya kiama.

Na imepokelewa kutoka kwake tena (a.s): Rekebisheni mwenendo yenu kwa walioachwa na wenzenu ili watendewe mema mtakao waacha baada ya kufariki kwenu.

Kwani moja ya natija ya kula mali ya yatima wa watu na kuwadhulumu, ni kudhulumu yatima kwa uonevu, hivyo ni wajibu kwa mwenye kuogopa jambo hili kujiepusha kudhulumu yatima wa wengine.

Imepokelewa kutoka kwa Imam Sadiq (a.s): "Mwenye kudhulumu Mwenyezi Mungu atamletea wa kumdhibiti au kukidhibiti kizazi chake au kizazi cha kizazi chake”.

Itaendelea.......





[1] Al- Nisaai/ 10.

[2] Al- Nisaai/ 2.

[3] Al- nisaai/ 9.

[4] Al- nisaai/ 9.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: