bayyinaat

Published time: 15 ,November ,2018      18:27:06
Licha ya kwamba, utawala wa Bani Abbas ulikuwa na ugomvi na Imam Askary AS, lakini mmoja wa mawaziri wa utawala huo aliyejulikana kwa jina la Ahmad bin Khaqan, alikiri juu ya
News ID: 358

Katika kipindi ambacho kilikuwa kimetanda giza la fikra potofu na aina kwa aina za uzushi, Imam Hassan AS alifanya hima na idili kubwa kubainisha uhakika na uhalisia wa dini tukufu ya Kiislamu kwa watu. Imam alikuwa akiwanywesha elimu Waislamu waliokuwa na kiu ya kutaka kuelimika kutoka katika chemchemi ya maarifa ya Ahlul-Beit AS.

Licha ya kwamba, utawala wa Bani Abbas ulikuwa na ugomvi na Imam Askary AS, lakini mmoja wa mawaziri wa utawala huo aliyejulikana kwa jina la Ahmad bin Khaqan, alikiri juu ya fadhila na utukufu aliokuwa nao Imam Hassan Askary kwa kusema kama ninavyonukuu: "Sijaona mtu mithili ya Hassan bin Ali mjini Samarra, Iraq. Hakukuwepo mtu mwenye sifa kama zake katika uchaji-Mungu, utakasifu na utukufu kati ya watu wote. Licha ya kwamba, alikuwa kijana, lakini watu wa kabila la Bani Hashim walikuwa wakimtanguliza mbele ya watu wote. Alikuwa na nafasi kubwa kiasi cha kupendwa na rafiki na adui.”

Utukufu wote huo Imam aliupata kutokana na unyenyekevu wake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kushikamana kwake na haki. Naye mtukufu huyo anasema: "Hakuna mtu mtukufu aliyetengana na haki ispokuwa alidhalilika na hakuna mtu duni na mdogo aliyefungamana na haki, isipokuwa atatukuzwa.”

Imepokewa katika hadithi tukufu kuwa, wakati Imam Hassan Askary AS alipokuweko gerezani, alikuwa akijishughulisha muda wote na ibada, kumkumbuka Mola wake na kumwelekea Yeye, kiasi cha kumuathiri askari aliyekuwa amewekwa kwa ajili ya kutoa adhabu na mateso kwa wafungwa. Siku moja maafisa wa utawala wa Bani Abbas walienda kumtembelea mlinzi wa jela aliyokuwa amefungwa Imam Hassan Askary AS.

Mlinzi huyo alijulikana kwa jina la Swaleh bin Waswif na kumtaka awe mkali na mgumu dhidi ya Abu Muhammad na kamwe asimpe utulivu hata kidogo mtukufu huyo. Mlinzi huyo aliwajibu maafisa hao wa Bani Abbas akiwaambia: Mnanitaka nifanye nini tena? Kwani humjasikia kuwa nimewapeleka askari wawili wakali zaidi kwenda kumtesa Abu Muhammad lakini kinyume na nilivyotarajia, watu hao wameathirwa sana na Abu Muhammad yaani Imam Hassan Askary AS na baada ya hapo si tu kwamba hawakumtazama kama mfungwa, bali waligeuka na kuwa ni watu wa kufanya ibada na kufunga na hivyo imani yao ikaimarika zaidi, hapo maafisa wale wa utawala wa Bani Abbas walitaka wale askari wawili waletwe mbele yao na wasailiwe, walipofika wakawaambia:

Ole wenu! Nini kimetokea mpaka mmeshindwa kumuadhibu mtu huyu yaani Imam Hassan, wale askari wakajibu kwa kusema: Mlitarajia tuseme nini mbele ya mtu ambaye mchana kutwa hufunga na usiku kucha hukesha katika kufanya bada? Mtu ambaye hajishughulishi na jambo jingine ghairi ya kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wakati alipokuwa akitutazama, tulikuwa tukiona haiba na utukufu wake.”

Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mu’utamad, mtawala dhalimu wa Bani Abbas wa wakati huo akafanya njama ambazo zingeweza kumuua shahidi Imam. Haukupita muda isipokuwa kiongozi huyo akamuwekea sumu ambayo ilimuua mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW baada ya kuugua kwa siku kadhaa. Mtumishi wa mtukufu huyo amenukuliwa akisema kuwa: Wakati Imam alipokuwa amelazwa akiwa mgonjwa katika hatua za mwisho wa maisha yake, alifahamu kuwa muda wa Swalatus Sub’h umewadia. Hapo alisema: "Ninataka kuswali.” Kisha nikamuandalia msala kitandani pake. Imam akatawadha na akaswali Swalatus Sub’h iliyokuwa swala yake ya mwisho katika kitanda chake na kisha akaaga dunia.” Innaa Lillaahi Wainnaa Ilayhi Raajiuna.

Imeandikwa na Salum Bendera.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: