bayyinaat

Published time: 15 ,November ,2018      18:35:07
Inaelezewa kwamba katika moja ya miaka ya utawala wa Mutawakkil kulitokea ukame mkali mno, na kipindi hicho imamu akiwa yupo kifungoni.......
News ID: 361

Imamu na Kiongozi wa Kikristo:

Miongoni mwa mambo ambayo yanatajwa sana katika kuelezea karama na utukufu wa Imamu Askariy ni pamoja na kisa kizima kilichojiri baina yake na baadhi ya viongozi wa Kiyahudi na Kinaswara.

Inaelezewa kwamba katika moja ya miaka ya utawala wa Mutawakkil kulitokea ukame mkali mno, na kipindi hicho imamu akiwa yupo kifungoni.

Basi Mutawakkil akaamrisha watu kwa imani zao tofauti kusimama na kuomba mvua, watu wakaitika wito na wakawa wakitoka kwa siku tatu mfululizo bila ya mafanikio yeyote. Ilipofika siku ya nne moja ya viongozi wa kinaswara akiwa na baadhi ya wanafunzi wake akatoka na kunyoosha mkono wake angani na hapo hapo mvua zikaanza kunyesha. Akawa akifanya hivyo kwa siku kadhaa mfululizo kiasi kwamba watu wakaanza kuingia shaka kunako usahihi wa dini zao nyingine kutokana na kitendo cha kasisi yule.

Mutawakkil naye baada ya kuona hali ile akachukua uamuzi wa kumtoa jela Imamu Hassan na kumwambia kwamba aangalie namna ambavyo umma wa babu yake umeangamia, kwa maana watu wote wameamua kuungana na dini ya Kinaswara. Imamu akamjibu kwa kusema "....Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nitaweza kuondoa hizi shaka katika nyoyo za watu...”.

Siku iliyofuata yule kasisi akatoka na watu wake kama kawaida, na Imamu naye akawa yupo na wafuasi wake wa kweli wakimwangalia atafanya nini yule Kasisi. Yule Kasisi akainua mkono wake kama kawaida kwa ajili ya kuomba mvua, ghafla Imamu akaamuru wanafunzi wake waukamate mkono wa yule Kasisi, na pindi walipofanya hivyo wakafanikiwa kutoka na kipande cha mfupa kutoka katika vidole vya yule Kasisi.

Kisha Imamu akamwambia yule Kasisi aendelee kuomba baada ya tukio hilo. Kila alipojitahidi kuomba hakikutokea kitu pamoja na kwamba tayari kulikuwa kumeshaweka alama za kunyesha mvua, kulibadilika na kuchomoza jua kali badala yake. Mutawakkil akashangaa sana na kumuuliza Imamu juu ya ule mfupa na siri zake. Imamu akasema kuwa ule ulikuwa ni mfupa wa moja ya mitume wa Mwenyezi Mungu ambao walifariki, na hakuna mbingu ambayo itaombwa kwa kutumia mfupa ule ila itafungua baraka zake.

Sababu ya Kifo chake:

Baada ya kuonekana kwamba Imamu amekuwa ni changamoto kubwa katika tawala za madhalimu, hasa ukizingatia kwamba anazidi kukubalika na watu wa aina zote na hivyo kutishia nguvu ya tawala hizo, Muutamad aliamua kupanga mipango ya kumuondoa Imamu duniani na ndipo alipofanikisha hilo kwa kuweza kumuwekea sumu iliyoondoka na maisha yake.

Na mnamo tarehe 8 Rabiul Awwal mwaka 260 H, Imamu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 28.

Katika mji wa Samarra nchini Iraq pembezoni mwa baba yake Imamu Hadi (as) ndipo ambapo amezikwa.

Inna Lillahi Wa Inna Ilaihi Rajiun.

Imeandikwa na Sh Abdul Razaq Bilal.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: