bayyinaat

Published time: 18 ,November ,2018      12:23:11
News ID: 370


Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kuwa, wanazuoni, wanaharakati wa kisiasa na wasomi kutoka nchi 100 za dunia wamealikwa kuja kushiriki Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ambao umepangwa kufanyika mjini Tehran.

Ayatullah Muhsin Araki ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran na kuongeza kuwa: "licha ya njama za madola ya kibeberu za kuvuruga umoja wa madhehebu za Kiislamu, wawakilishi 350 wa nchi 100 watashiriki katika mkutano wa 32 wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran."

Ayatullah Muhsin Araki ameashiria hatua zilizochukuliwa katika kukurubisha madhehebu za Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu na kusema kuwa, kumekuwepo njama za madola ya kibeberu na kiistikbari za kuvuruga umoja wa Kiislamu duniani. Aidha amesema kuwa: "Marekani inataka kuzusha wimbi la upinzani dhidi ya Iran kwa kutumia vibaraka wake kama vile watawala wa Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel.

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 hadi 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitangaza kipindi cha tarehe mbili hizi kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: