bayyinaat

Published time: 23 ,November ,2018      20:59:06
News ID: 374

Watoto zaidi ya 84,700 wa Yemen wamepoteza maisha kutokana na makali ya njaa na utapiamlo, tangu Saudi Arabia ianzishe vita dhidi ya nchi hiyo maskini.

Ripoti iliyotolewa wiki hii na Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Watoto la Save The Children imesema kuwa, watoto hao wamefariki dunia baada ya kukumbwa na utapiamlo wa kiwango cha juu na kisha kukosa matibabu, tangu Aprili mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka huu.

Tamer Kirolos, Mkurugenzi wa Save The Children nchini Yemen huku akinukuu takwimu za Umoja wa Mataifa amesema, "Tumeshtushwa na habari kwamba, takriban watoto 85,000 huenda wameaga dunia kutokana na makali ya njaa tangu vita dhidi ya nchi yao vianze. Kwa kila mtoto anayeuawa kwa bomu na risasi, kuna makumi ya wengine wanafariki dunia kutokana na njaa, jambo ambalo bila shaka linaweza kuzuilika."

Hayo yanajiri katika hali ambayo, ripoti mbalimbali za Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) zimekuwa zikitahadharisha kuhusiana na matokeo mabaya na maafa yanayosababishwa na kuendelea hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake huko nchini Yemen.

Aidha ripoti mbalimbali zinaeleza kwamba, zaidi ya watoto milioni 11 wa Yemen wanakabiliwa na uhaba wa chakula, maradhi na ukosefu wa makazi.

Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: