Haja ya kuwepo viongozi wa Kimungu
miongoni mwa mambo ambayo yanakuwa
yakiulizwa sana kutokana na sababu moja au nyingine ni kwamba je, kuna ulazima
wowote wa Mwenyezi Mungu kutuma watu ambao ni kama sisi kwa ajili ya kuja
kutufundisha?, kwani akili na uelewa wetu hautoshi kuweza kuyajua yale ambayo
wao huja kutufundisha?, kwa sababu mambo ambayo Mitume wanakuja nayo hayatoki
katika hali mbili zifuatazo:
(a)
Kwamba ni mambo ambayo akili zetu zinaweza kuyafikia na kuyatatua.
(b)
Ni mambo ambayo akili zetu haziwezi kuyafikia na kuyatatua.
Tukiichunguza hali ya kwanza bila
shaka kuna natija ambayo tunafikia ambayo ni: kama haya mambo ambayo wanakuja
nayo mitume kuna uwezekano wa akili yetu kuyafikia na kuyatatua, basi kuna
faida gani ya wao kuja?.
Hali kadhalika hali ya pili pia kuna
natija ambayo tunafikia ambayo ni : kama haya mambo ambayo wanakuja nayo
hayawezi kufikiwa na akili zetu, basi kwanini waje nayo? Maana nafsi ya
mwanadamu siku zote hupenda kitu ambacho inajua uhakika wake. Lakini mbali na
hayo kuna jambo ambalo ndilo lenye kuumiza zaidi nyoyo za wanadamu, ambalo ni
kwanini wanadamu wote wawe chini ya mamlaka ya mwanadamu mwenzao tena ambaye ni
mmoja?.
Sasa ili kuweza kupata majibu ya
maswali haya ni lazima kwanza tuchambue baadhi ya mambo ambayo ndio yatatupa
mwangaza kwa kila ambacho kinaweza kuwa ni kizuizi au sababu ya kujiuliza
maswali haya.
1.
Ni lazima kwanza tukubali kwamba elimu na hata akili zetu zina
mapungufu makubwa sana katika kufahamu na kudiriki kila jambo, na aili
kuthibitisha hili hebu tuangalie pamoja na kwamba ulimwengu umekuwa ni wenye
kuendelea mno katika nyanja za elimu, lakini pamoja na hayo kama tutaamua
kupima idadi ya mambo tunayoyajua na mambo tusiyoyajua, tutakuta kwamba idadi
kubwa itaangukia katika mambo tusiyojua, hii ina maana kwamba mambo tunayoyajua
ni machache kuliko mambo tusiyoyajua.
Kisha hebu tuwe wakweli na nafsi
zetu, je ni sahihi kugawanya mambo katika vipengele viwili tu, yaani kusema
kwamba mambo yote ima yawe ni yenye kufikiwa na akili au yasiyofikiwa na
akili?, kwani hatuwezi kusema kwamba mambo yanagawanyika katika makundi matatu,
kuna ambayo yanafikiwa na akili na yamejulikana, kisha kuna ambayo yanafikiwa
na akili lakini bado hayajajulikana, na mwisho kuna ambayo hayajulikani kabisa
kwamba yanafikiwa na akili au la?.
Kama jawabu litakuwa ndio
inawezekana kukawa na vigawanyo hivi katika mambo, basi kwa urahisi tunafikia
katika natija ya kwamba hawa mitume wao huja na mambo ambayo hayajulikani kwa
watu na pia ni yenye kufikiwa na akili za hao watu, kwani ni kinyume cha malengo kwamba Mitume waje na
mambo ambayo hayaendani wala hayafikiwi
na akili ya mwanadamu, na kama itakuwa watu wanayaona ni kinyume na
akili basi huu ni ule upungufu wao na wala si upungufu kwa Mtume au jambo
lenyewe kama tutakavyokuja kubainisha hapo baadaye.
Kwa minajili hii basi, kila ambaye
anasimama na kusema kwamba hakuna haja wala faida yeyote ya kuwepo Mitume (kama
kundi la Barhama huko India na kwengineko) basi kwa uhakika itakuwa
hawajafahamu kwamba akili na uelewa mwanadamu hauwezi kufikia na kuelewa kila
jambo, na mfano wake ni mfano wa mwanafunzi wa chekechea ambaye ndio kwanza
amejifunza silabi zote na kuona kwamba hana haja tena ya mwalimu kwani
ameshajua.
2.
Kwa ambaye anaona kwamba swala la kuwepo Mitume litapelekea
binadamu wote kuwa katika utawala na mamlaka ya binadamu mmoja, ni lazima
atambue yafuatayo: tunapozungumzia mtume basi ni wazi kwamba tunazungumzia
binadamu ambaye ana mahusiano ya karibu mno na Mwenyezi Mungu kuliko hao
binadamu wengine, na kuwa kwetu chini yake basi ni kwa sababu tu ya hii sifa
ambayo sisi hatuna, sasa je katika hali kama hii bado itabakia kwamba ni jambo
baya?.
Kwa mantiki hii tunafikia katika
natija ya kwamba kukataa uwepo wa Mitume kwa vigezo kwamba sisi wenyewe
tunaweza kuyafikia hayo mambo ambayo wanakuja kutufundisha, au kwa kigezo
kwamba kuja kwao kuna maanisha kwamba binadamu wote tutakuwa chini ya mtu
mmoja, ni mambo ambayo hayana mashiko wala uhakika ndani yake. Na hii ni
kutokana na kwamba siku zote akili ya mwanadamu haiwezi kufikia kila kitu, na
hawa mitume ndio ambao wanakuja kumfunza asiyoyajua kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Pia kuwa chini ya watu kama hawa sio jambo baya, kwani wana kitu ambacho
wanatuzidi na hatuna, nacho ni kwamba wao wapo karibu sana na muumba na wana
elimu ambayo sisi hatuna, na nafsi ya mwanadamu inahukumu ubaya endapo tu
itakuwa chini ya ambaye wanalingana kila kitu au amemzidi baadhi ya mambo.
Itaendelea......