Je uchambuzi juu ya swala la Uimamu
ulianza lini?
Katika maswala ambayo yamekuwa
yakizunguka katika vichwa vya Waislamu ni swala la kujadili na kutafuta ni nani
ambaye anafaa kuwa Imamu na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume. Na ni kwanini
Waislamu wamekuwa ni wenye haja na shauku sana katika kujadili jambo hili?.
Kwani kuna sababu gani iliyopelekea mpaka kuanza kupatikana majadiliano na hata
tafiti mbalimbali za nani ambaye anafaa kuwa Imamu baada ya mtume?.
Jawabu la swali hili tunaweza
kulipata endapo tu tutarejea hali ya Waislamu baada ya kufariki dunia bwana
Mtume Muhammad (saww), kwani ni jambo ambalo lipo wazi kwamba baada ya kufariki dunia tu Bwana Mtume (saww) umma uligawanyika
makundi mawili makuu, na kila kundi moja likiwa na msimamo na itikadi yake juu
ya ambaye anafaa kuwa kiongozi na Imamu baada ya Mtume (saww). Makundi hayo
pamoja na misimamo yao ni kama ifuatavyo;
1.
Kundi ambalo linaamini kwamba Bwana Mtume hakuacha kiongozi baada
yake, na kwamba swala la umma kuwa na kiongozi lipo mikononi mwa umma na
Waislamu wenyewe, wao ndio wana haki ya kumchagua wamtakaye ili awe kiongozi na
Imamu wao.
2.
Kundi ambalo linaamini kwamba kazi ya kuchagua kiongozi wa Waislamu
baada ya Mtume ipo mikononi mwa Mwenyezi Mungu (swt), kwani huyu kiongozi ni
lazima awe na sifa ambazo alikuwa nazo yule aliyekuwa kabla yake mfano sifa ya
kutofanya madhambi na nyinginezo, na kwakuwa sisi wanadamu hatuna uwezo wa
kuweza kutambua kwamba huyu ana sifa hizo au la, inakuwa kwamba ni lazima Imamu
na kiongozi huyu aainishwe na Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake.
Hivyo basi na sisi katika mada hii
tutajaribu kufuatilia jambo hili kwa ukaribu mno na kuweza kufikia katika
natija sahihi huku tukitumia Quran, Sunna pamoja na historia sahihi ya Uislamu,
lakini kabla ya kuanza hilo ni lazima tutambue baadhi ya mambo muhimu ambayo ni
mwongozo wa kutambua jambo hili. Mambo yenyewe ni yafuatayo:
a.
Je, ni kweli kuzungumzia jambo hili husababisha tofauti baina ya
Waislamu?.
imekuwa
ni jambo lenye kuzoeleka sasa katika jamii zetu kwamba, kili isikikapo jambo la
kujadili juu ya Imamu na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume basi watu wote
husimama na kusema kwamba jambo hili halifai kujadiliwa wakati huu, kwani huu
ni muda wa Waislamu kushikamana na kuwa wamoja, na kwamba swala la kujadili
Uimamu baada ya Mtume ni katika mambo ambayo husababisha mfarakano na
mgawanyiko wa Waislamu. Lakini sidhani kama mtazamo huu ni sahihi kabisa, na
hii ni kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza:
jambo ambalo husababisha mfarakano na mgawanyiko na hata chuki baina ya
Waislamu ni kujadili mambo haya hali ya kuwa kila mmoja hana moyo safi wa
kutaka kuelewa au kujua ukweli, bali unakuta kwamba mtu anajadili jambo hili
huku moyo ukiwa haupo tayari katika kusikia au kukubali ukweli, sasa inapotokea
akaambiwa ukweli upo hivi na hali ya kuwa moyo wake hautaki kusikia na kuamini
kwamba hayupo sahihi hapo ndipo ambapo mfarakano unapatikana. Na wala
haiwezekani mfarakano ukapatikana endapo kila mmoja ataingia katika mjadala wa
jambo hili huku akiwa na moyo safi wa kuwa tayari kukubali ukweli hata kama
utakuwa dhidi yake.
Pili:
inawezekana sababu ya mfarakano baina ya Waislamu ikawa ni kutofahamiana wao
kwa wao, kwa maana ya kwamba utakuta kundi hili lina amini imani fulani na
dalili zake zikawa ni fulani, lakini maadui wa Uislamu wakasimama kidete
kuhakikisha kwamba zile dalili zinabadilishwa maana yake na kupelekwa upande wa
pili ambao hauamini ambayo yanaaminiwa na upande wa kwanza. Kwa mfumo huu bila
shaka lazima kutakuwa na mizozo ya kwanini na kwanini huku ikidhanika kwamba sababu
ya mizozo ile ni kujadili tu maswala mfano wa swala hili la Uimamu.
Mfano
mzuri ni ule ambao tunakutana nao kila siku katika maisha yetu, ambapo tunakuta
kwamba kuna kundi la Waislamu linalojitahidi kuaminisha umma kwamba, baina ya
Waislamu kuna ambao wana Quran yao tofauti na Quran iliyozoeleka kwa Waislamu
wote. Sasa mambo kama haya hua ndio sababu ya mizozo na mifarakano kwa Waislamu
na sio kujadili mambo yanayohusu Uislamu kwa moyo safi na nia njema.
b.
Nini maana ya Uimamu?
Imamu
kama ambayo inaelezwa maana yake ni yule ambaye anafuatwa katika Uislamu na
yeye anawaongoza wanaomfuata. Isipokuwa tu itakuja tofauti kwa upande wa
dhehebu la Shia (ithna asharia) kwamba
wao wanaamini ya kuwa huyu Imamu ni lazima awe ni maasumu (ambaye hafanyi
dhambi) na kwamba Imamu huyu maasumu haina maana kwamba atakuwa ni kiongozi
katika mambo ya dini tu, bali anakuwa ni kiongozi katika kila jambo ambalo
linawahusu Waislamu. Na hii ni maana ambayo hatuipati katika dhehebu nyingine
za Kiislamu, kwani wao huamini kwamba Imamu au kiongozi wa Kiislamu anakuwa ni
kiongozi wa jamii ya Kiislamu na maswala ya kidini tu, ama mambo mengineyo
yanakuwa nje ya utawala na mikono yake.
ndugu
msomaji mpaka kufikia hapa tunakuwa tumeweza kutambua ni ipi maana ya Imamu,
kama ambavyo pia tunakuwa tumeweza kutambua kwamba swala la kujadili Uimamu si
katika maswala ambayo husababisha tofauti baina ya Waislamu, lakini ni kwa
sharti tu kwamba swala hili lijadiliwe hali ya kuwa tupo na nia safi na moyo wa
kukubali ukweli hata kama utakuwa dhidi yetu.
Tukutane
katika makala ijayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.