Kwa jina
la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu
Mahusiano baina ya Uislamu na dini zilizopita
Miongoni mwa neema kubwa ambazo Mwenyezi Mungu
amewajaalia waja wake, ni kwamba amewaumba katika hali ya kwamba wao ndani ya
nafsi zao wana hali ya kumjua na kumkubali Mungu, na hali hii ipo kwa kila
mwanadamu hata kama atakuwa ni mwenye kupinga kwa maneno au matendo yake,
lakini ni kwamba kimaumbile ni mwenye kukubali uwepo wa nguvu iliyo juu ya kila
kitu. Lakini kutokana na kwamba hali hii ni hali ambayo bado haijafafanuliwa
zaidi kwa mwanadamu huyu ndio tunakuta kwamba mwenyezi mungu anatuma Mitume ili
kuja kuisherehesha hali hii pamoja na kuthibitisha kwamba ni kweli ipo
isipokuwa ili uitambue ni lazima upite katika misingi fulani. Na miongoni mwa
misingi hiyo ni kama:
1.
Kumpwekesha
Mungu na kutomshirikisha na yeyote
2.
Kumuabudu
yeye peke yake pasi na mwingine
3.
Kulinda na
kuhifadhi mambo ya watu pamoja na kutosababisha uharibifu
4.
Kulingania
watu kuelekea katika tabia zilizo bora. Na mfano wa mambo mengine mengi ambayo
huja kuelekezwa na Mitume.
Kisha Mwenyezi Mungu kwa matakwa yake akaamua
kwamba dini ya Islamu iwe ndio dini ya mwisho na ambayo inakuja kukamilisha
dini zote zilizopita, na kwamba dini zilizopita au mitume pamoja na ujumbe zao
ni kwamba zilikuwa na muda maalumu tu. Lakini hii haina maana kwamba dini ya
Islamu ni dini ambayo imekuja kupinga na kubatilisha dini zilizopita, au kuja
kusema kwamba dini hizo hazikuwa na maana wala mashiko, na ndio maana katika
makala hii tunataka kubainisha kwamba Uislamu kama Uislamu una mambo ambayo
yanashikamana na yanaendana na dini zilizopita, kwani lengo la Uislamu ni kuja
kukamilisha dini zote zilizokuwa kabla yake. Na mambo hayo ni kama ifuatavyo:
1.
Msingi na
asili ya dini zote ni moja
hii ikiwa na maana kwamba, pamoja na kuwa dini
hutofautiana zama na nyakati au hata Mtume ambaye huja nayo, ila tunakuta
kwamba dini hizi zote zinakutana katika asili na msingi. Na msingi huo ni
kwamba zote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu mmoja, (lakini hapa ni lazima ifahamike
kwamba dini tunazozikusudia ni dini ambazo zinatoka kwa mwenyezi mungu na sio
dini za kuundwa na wanadamu wenyewe) na katika kubainisha hilo tunakuta
Mwenyezi Mungu anasema:
شَرَعَ
لَكُمْ مِنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ
وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا
الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ ....
" Na amekuwekeeni sheria ambayo aliiweka kwa Nuh, na hayo ndio
ambayo tumekupatia wewe na Ibrahimu na Mussa na Issa (Yesu) ya kwamba muwe ni wenye kusimamisha dini na
wala msiwe ni wenye kutofautiana......” surat Shuura aya ya 13.
Kwa hiyo kwa msingi huu ni
kwamba imani ya kweli haiwi tu kwa kusadikisha yale ambayo amekuja nayo mtume
wa zama zako, bali pia ni kusadiki ambayo walikuja nayo mitume wa kabla pia.
2.
Malengo ya dini zote ni mamoja
Hapa ikiwa na maana kwamba
dini zote pamoja na kutofautiana kwake nyakati na muda, ila zinakuja
kukutana katika malengo yake. Kwani kama ambavyo ipo wazi ni kwamba dini zote
zinakuja kwa lengo la kumwongoza mwanadamu na kuhakikisha kwamba anafikia
katika ukamilifu ambao kwao aliweza kuumbwa.
3.
Dini zote zina nembo ya Uislamu
Naam na wala sio uongo,
kwani ni jambo ambalo tunalikuta kwa Mitume iliyopita pia tofauti na mtume
Muhammad (saww), na hii ndio maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema :
إِنَّ الدِّينَ عِنْدَ اللَّهِ الْإِسْلَامُ
"hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu”
Al imran aya ya 19.
Na ili kuthibitisha ya
kwamba hata katika dini za mitume iliyopita kulikuwa na nembo ya Uislamu,
yatutosha kurejea kauli za baadhi ya mitume walipokuwa wakielezea malengo na
falsafa ya dini walizokuja nazo. Angalia mtukufu nabii Nuhu katika maneno yake
baada ya kubainisha malengo yake anasema:
وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ
"na nimeamrishwa niwe ni mwenye kujisalimisha (Mwislamu)
Surat Yunus aya 72
Pia tunamkuta Nabii Yusuf
katika dua alizokuwa akiomba ni pale aliposema:
تَوَفَّنِي
مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ
"ewe mola wangu nifishe hali ya kuwa nikiwa Mwislamu na uniweke
pamoja na walio wema” surat Yusuf aya ya 101.
Na kauli nyingi mno ambazo
zimepokelewa kwa Mitume wengine kama vile Suleiman, Ibrahim, Ismail, Yakob na
wengineo, kauli ambazo zote zina maana ya kuashiria kwamba katika ujumbe wao
kulikuwa na nembo ya Uislamu.
Lakini ndugu msomaji, swala la
muhimu kujua hapa ni kwamba, Uislamu ambao unamaanishwa na pia ulikuwa katika
kila dini ni upi? Maana isije tukaelewa vibaya na mwisho wake tukaangukia
katika janga kubwa la kupinga dini nyinginezo na kusema kwamba hazijulikani kwa
Mwenyezi Mungu.
Ili kuweza kujua na kufahamu
maana ya Uislamu ambao ulikuwa katika kile dini basi usiache kuungana nami
katika makala ijayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu (swt)
Sh Abdul Razaq Bilali.