MWENYEZI
MUNGU (S.W) KAMFADHILISHA MWANADAMU
' KWA FADHILA YA USAFI
Ndugu msomaji, kwa hakika kama ambavyo akili
huweza kumtofautisha mwanadamu na viumbe wengine, hivyohivyo usafi. Na hii ni
miongoni mwa fadhila kubwa alizobahatika kufadhilishwa kwazo mwanadamu kuliko
viumbe wengine kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w):
﴿وَفَضَلناهُمْ
على كثيرٍ مِما خلقنا تفضيلاً ﴾
"na
tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba"
Miongoni mwa mafunzo ya dini tukufu ya
Kiislam ni 'usafi wa kimwili na kiroho'. Naamini kwamba kila mtu atakuwa
wa kwanza kukubaliana na mimi katika kauli hii kwamba 'dini tukufu ya Kiislam
ni dini safi'. suala hilo liko wazi mno kwa wanadamu wote waliotangulia
waliopo na watakao fuatia. Na ndio maana utaikuta dini hii inasisitiza zaidi
usafi.
Allah (s.w) baada ya kumuumba mwanadamu kwa
maumbile mazuri na sura nzuri kama zisemavyo Aya tukufu akaendelea kumkirimu
mwanadamu huyu kwa kumuumbia vitu ambavyo kwavyo mwanadamu anaweza kutengeneza
mavazi au nguo ili ahifadhi mwili wake, anasema Allah (s.w):
﴿يا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنزَلْنَا عَلَيْكُمْ
لِبَاساً يُوَارِي سَوْءَاتِكُمْ وَرِيشاً ﴾
"Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu,
na nguo za pambo…."
(
Qur`an-7/26).
Mwenyezi Mungu hakufanya hivyo isipokuwa
alitaka mwanadamu huyu aonekane katika mandhari iliyokuwa nzuri ili aende sawia
na maumbile yake, na ili kumtofautisha na viumbe wengine ambao hawakubahatika
kuteremshiwa nguo (kama isemavyo Aya hii) au kuumbiwa vitu ambavyo wanaweza
kutengeneza nguo kutoka katika vitu
hivyo ili wahifadhi miili yao.
Na iko wazi kwamba uzuri wa dhahiri ya
mwanadamu hautakamilika pasina kulitilia umuhimu usafi, kama ambavyo uzuri
wa batini (au uzuri wa nafsi) haupatikani pasina kulitilia umuhimu uchamungu
ambao maana yake ni "kutii amri zote za Mwenyezi Mungu (s.w) pamoja na
kuacha yote aliyokukataza Mola wako".
Ili
uwe msafi zaidi kiroho ni lazima uwe mchamungu kwa maana hiyo tuliyoitaja hivi
punde. Na hivyohivyo ndivyo usafi wa dhahiri au mwonekano wa nje wa mwanadamu
hupendeza kwa kutilia umuhimu usafi wa mwili, kwa maana kwamba unatakiwa
uwe na tabia ya kupenda kuvaa nguo nzuri na safi, uwe na tabia ya kupenda
kulala katika sehemu iliyokuwa safi, na uwe na tabia ya kupenda kuishi katika
sehemu iliyokuwa safi yenye mazingira safi.
Hivyo usafi kwa mwanadamu tutauzungumzia
katika sekta hizi zifuatazo:
Usafi kwa mtu binafsi (mwili wake na mavazi
yake).*
*Usafi katika jamii yake anayoishi
*Usafi
katika taifa lake.
USAFI
UNAOMHUSU MTU BINAFSI
Tumesema kwamba miongoni mwa neema za
Mwenyezi Mungu (s.w) kwa Mwanadamu ni kumtakasa mwanadamu huyu na kumfanya
awe msafi kuanzia usafi wa kiroho (au usafi wa bitini na wa ndani ya
nafsi), hadi usafi wa kimwili (nikimaanisha usafi wa dhahiri wa mwanadamu).
Katika Suuratul Maidah, Aya ya 6, Mola wetu
Mtukufu anasema:
﴿مَا يُرِيدُ اللـه لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِنْ حَرَجٍ وَلكِن يُرِيدُ
لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾
"Mwenyezi Mungu hataki kukutieni katika taabu; bali anataka
kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru"
Dini tukufu ya Uislamu inasisitiza usafi wa
aina zote mbili, kwamba Mwislamu anatakiwa kuwa msafi kiroho, kwa kuilea nafsi
yake iwe ni yenye kumtii Mwenyezi Mungu (s.w) katika mambo yote pasi na
kwanini, pia iwe ni nafsi yenye kuheshimu haki za wengine na kuishi na watu
vizuri, nafsi isiyokuwa na chuki wala kinyongo, iwe ni nafsi yenye uwezo wa
kusamehe inapokosewa na kuomba msamaha inapokosea, nafsi yenye huruma, upole na
ustahamilivu, n.k., na hivyo ndivyo usafi wa kiroho unavyotimia.
Ama kuhusiana na usafi wa dhahiri ambao
ndio muhimili mkubwa wa mada hii Uislamu
unahimiza siku zote Mwislamu azingatie usafi wa mwili wake, na hata nguo zake
anazozivaa pamoja na chakula chake anachokula, tunatakiwa kuhakikisha vyote hivyo vinakuwa katika hali ya usafi.
Mwanadamu (Mwislamu) kama unavyotakiwa kuwa
msafi wa kimwili na mavazi yako hivyohivyo ndivyo unatakiwa kula chakula bora
na safi kilichohalalishwa ,na hili ni miongoni mwa mambo ambayo Allah (s.w)
amemtaka Mtume Muhammad (s.a.w.w) ayafanye.
ukirudi katika historia ya maisha ya Mtume
(s.a.w.w) utakuta ni Mtume ambaye hakutosheka na kuwaamrisha wanadamu mema na
kuwakataza maovu tu, bali pia alifanya kazi kubwa ya kuwabainishia na kuwahalalishia vilivyokuwa halali na safi,
na kuwaharamishia kinyume na hivyo, katika Suuratul Aa'raf,Aya ya
157 Mwenyezi Mungu (s.w) anasema namna hii:
﴿وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَآئِثَ﴾
"….. na anawahalalishia
vitu vizuri, na kuwaharamishia vitu vichafu"
Kunako usafi wa mwili ni pamoja na
kuzingatia suala la kuoga, kuweka nywele zako safi, kukata au kupunguza
kucha ,kuzingatia suala la kupiga mswaki ,kweka kiatu chako safi, pamoja
na mavazi yako (au nguo zako) kuonekana katika mpangilio uliokuwa mzuri. n.k.
Ikiwa wewe ni Mwislamu anayependa na
kutarajia kuingia peponi ,basi zingatia usafi wa ndani ya nafsi yako, usiwe
kiburi katika nafsi yako maana utakuwa unaichafua kwa kufanya hivyo, pia
unatakiwa uzingatie usafi wa kimwili ,kwa kuvaa mavazi safi na kiatu chako
unapiga dawa king'ae ,kwa kufanya hivyo utakuwa unamfurahisha Mwenyezi Mungu(
s.w) na bila shaka ukimfurahisha Mola wako utakuwa umefanikiwa kuingia kwenye orodha
ya wale watakao ingia Peponi, kwani pepo
ya Allah (s.w) ni safi na watakaoingia ndani yake ni wale waliozingatia usafi .Na
hivi ndivyo alivyosema Mtume (s.a.w.w), Ibn Mas-uud amesema kwamba Mtume
(s.a.w.w) amesema:
( لا يدخل
الجنة من كان في قلبه مثقال ذرة من كبر، فقال رجل: إن الرجل يحب أن يكون ثوبه حسنا
ونعله حسنا، قال –يعني النبي صلى الله عليه واله وسلم-: إن الله تعالى جميل يحب
الجمال، الكبر بطر الحق، وغمط الناس.)
"Hataingia peponi yeyote atakaye kuwa
na chembe ndogo ya kiburi katika moyo wake, Mtu mmoja (akashangaa sana
alivyosikia kauli hii ya mtume -s.a.w.w.-mana yeye alikielewa kwamba kuvaa nguo
nzuri na safi, pamoja na kuvaa kiatu safi ni aina moja wapo ya kiburi) akamuuliza
Mtume s.a.w.w- kwa kusema: Kuna Mtu (fulani) ana tabia ya kupenda nguo zake
ziwe safi, pia anapenda kiatu chake kiwe
safi!,
(Vipi mtu
huyu, naye hataingia peponi?), Mtume (s.a.w.w) akamjibu kwa kusema:
Hakika Mwenyezi Mungu ni msafi, na anapenda
usafi, kiburi ni majivuno na maringo yaliyo dhidi ya haki kwani humfanya mtu
awe na dharau na kutokuwa tayari kuitambua haki ya mtu mwingine"
Mwenyezi Mungu anapokuwa amekuneemesha kwa
neema fulani, basi hupendezwa sana kuziona athari nzuri za neema hiyo
aliyokupa, kwa mfano neema ya akili, atafurahi sana Mola kuona ikiwa utaitumia
akili yako vizuri ,na hivyohivyo ikiwa utazingatia usafi hakika Mola wako
atafurahi mno kuona ni jinsi gani unavyoithamini neema yake ya kukuumba vizuri
na kukupa sura nzuri ikiwa utajali usafi wa maumbile yako (mwili wako).