Hivyo basi tunatakiwa kuvaa vizuri, nguo
safi, zinazopendeza na kutufanya tuonekane vizuri, ikiwezekana unatia na
manukato hasa unapokuwa mbele ya Mola
wako ukifanya ibada, itapendeza sana ikiwa utaingia katika swala ukiwa msafi
mwenye mavazi safi, na hivi ndivyo Waislam tunavyotakiwa tuwe, kwani amesema:
﴿ يَا بَنِي آدَمَ خُذُواْ زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ
وكُلُواْ وَاشْرَبُواْ وَلاَ تُسْرِفُواْ إِنَّهُ لاَ يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ﴾
"Enyi wanaadamu (Waislamu)! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala
wakati wa ibada, na kuleni (vizuri), na kunyweni (vizuri) na wala msifanye
ubadhirifu, Kwa hakika Yeye hapendi wabadhirifu".
Hivyo itakuwa ni suala la msingi ikiwa
tutaitumia neema ya maji tuliyopewa na Mola wetu kwa kufanya usafi wa mwili na
mavazi, kama kuoga, kufua nguo zetu, n.k. na iwapo hatutafanya hivyo basi tujue
kwamba badala ya kumfurahisha Mola wetu tutakuwa tunamuudhi.
Imepokewa riwaya kutoka kwa Jaabiri anasema
kwamba ;
"أتانا رسول الله صلى الله عليه وسلم زائراً، فرأى رجلا شعثاً، قد تفرق
شعره، فقال: ما كان يجد هذا ما يسكن به رأسه"
"siku moja tulimzuru Mtume (s.a.w.w), Mtume
akamuona mtu (miongoni mwa waliomjia) ambaye nywele zake zilikuwa zimatawanyika
tawanyika,akasema kwa kuuliza (s.a.w.w): Mtu huyu hakupata kitu cha kumuwezesha
kuziweka nywele zake safi zikatengamaa"?!.
Pia amepokea Abi Ahwaswi kutoka kwa baba
yake kuwa amesema:
( أتيت رسول
الله صلى الله عليه واله وسلم وعلي ثوب درن، فقال لي: "ألك مال"، قلت
نعم. قال: من أي المال؟ قلت من كل المال، قد أعطاني الله من الإبل والغنم والخيل
والرقيق. قال: فإذا آتاك الله مالا فلير أثر نعمة الله عليك وكرامت.)
"Nilimjia Mtume (s.a.w.w) ilihali katika nguo
yangu kukiwa na uchafu, Mtume akaniambia: Una mali?, nikasema: ndio, akasema
(s.a.w.w):ni mali zipi ulizokuwa nazo?, nikasema: mali zote, kwa hakika Mwenyezi
Mungu -s.w- amenipa (mifugo mingi sana) Ngamia, Kondoo na Mbuzi, Farasi pamoja
na watumwa. Mtume (s.a.w.w) akasema: Mwenyezi Mungu anapokupa mali basi
jitahidi sana aone athari za neema zake alizokupa pamoja na fadhila zake
kwako."
Riwaya hii inatubainishia ni jinsi gani
suala la usafi lilivyopewa umuhimu mkubwa katika Uislamu, ukiwa mchafu wa mavazi
basi utakuwa si mwenye kushukuru neema za (Mwenyezi Mungu (s.w) ,kwani unaweza
kujali mwili na kuuweka katika hali ya usafi lakini hufanyi hivyo ,kakupa maji
na unaweza kuoga na kufua nguo zako na kuziweka safi lakini hufanyi hivyo, na
hakuna shaka kuwa kufanya hivyo ni kukufuru neema za mola wako.
Na usafi sio wa mwili peke yake bali pia tunatakiwa tufanye usafi
kwenye majumba yetu na sehemu tunazoishi, tuyapambe majumba yetu kwa usafi yawe
mazuri, mazingira yetu yavutie, tukifanya hivyo basi tutakuwa ni miongoni mwa
wale ambao Allah (s.w) amewazungumzia kwa kuwasifu akisema :
﴿ فِيهِ
رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا وَاللـه
يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ﴾
…..Humo wamo watu
wanao penda kujitakasa (na kuwa wasafi), na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaojitakasa".
(Tazama katika Suratut- Tawbah: Aya ya 108.)
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anazungumzia kunako tohara
na usafi kwa ujumla, hivyo ili tufanikiwe na kuwa miongoni mwa wale wanaopendwa
na Mola wao ,tunatakiwa tupende usafi na tupende kuwa wasafi.
USAFI WA JAMII
Ikiwa Mtu au Mwislamu atazingatia usafi
unaomhusu yeye binafsi kuanzia mwili wake na mavazi yake n.k, basi ataweza
kuzingatia usafi wa jamii yake anapoishi. Na usafi wa jamii ni tofauti na usafi
wa kimwili unaohitaji vitu kama kuoga ,kuvaa nguo safi na nzuri kuweka nywele
safi kukata kucha n.k, bali katika sehemu hii ninaposema usafi katika jamii
ningependa kumaanisha usafi wa mazingira katika jamii unayoishi.
Hakikisha mazingira ya jamii yako yawe
safi, na uchukie utakapomuona mtu anachafua mazingira maana atakuwa anaichafua
jamii yako.
Kuna watu utakuta wana tabia ya kuchafua
mazingira ,kama vile kujisaidia hovyo sehemu zisizotakiwa ,pia kuna watu
wengine hawajui nini maana ya kutunza mazingira, ni waharibifu wa mazingira, kwa
hakika hali hii hutokana na kutojua au kutambua thamani ya utunzaji wa
mazingira ,mtu wa namna hiyo itakuwa ni vigumu kwake kutunza hata usafi wa
mwili wake.
Msafi ni yule ambaye usafi wake hauishii
kujali mwili wake na kuvaa vizuri, bali msafi ni yule ambaye hupenda kuwa safi
yeye binafsi pia mazingira ya jamii yake. utamkuta mtu ni mwenye kufanya usafi
hata wa njia na sehemu wanazo pumzikia watu, maana anajali, hajisikii furaha
kuona njia ikiwa na miba, ama mchafu yeye hana habari na hajali , bali utamkuta
ni bingwa wa uchafuzi wa mazingira na njia za watu, kwa hakika ada mbaya sana
ni mtu kutupa takataka kwenye njia za watu, mwenye kuchafua barabara ambapo
husababisha njia hizo kuwa na harufu mbaya inayokera watu, yeyote atakayefanya hivyo
basi ajue kwamba anailetea maudhi jamii yake, na nchi yake kwa ujumla.
Mtume (s.a.w.w) anatwambia kwamba:
(التسبب في اتساخ الطريق وأذى المارة سيئة تنقص من درجة الإيمان
الكامل)
" kusababisha uchafu katika nchi na kuwaudhi
wapita njia ni jambo baya sana ambalo linapunguza daraja ya imani kamili,".
Mtume (s.a.w.w) anasema:
" أتقو اللاعنين ، قيل : وما اللاعنان؟ قال : الذي يتخلىّ في
طريق الناس أو ظلهم "
"Jitenge na walio laaniwa Wawili,
Mtume akaulizwa: ni watu gani hao wawili walio laani: Mtume (s.a.w.w) akasema:
Anayejisaidia katika njia wapitazo watu au anayejisaidia katika sehemu za
vivuli vya watu kwa ajili ya kupunga upepo na kupumzika
itaendelea…: