bayyinaat

Published time: 29 ,January ,2024      09:02:53
Nasaha ya Uislamu kwa Anayetaka Kuoa (sehemu ya 2)
3. Ukomavu wa kiuchumi Ukomavu wa kiuchumi inamaanisha kuwa na uwezo na ujuzi wa kutafuta pesa, kuhifadhi pesa hizo, usimamizi mzuri wa pesa hizo na uendeshaji mzuri wa gharama za maisha. Katika baadhi za tamaduni, mara nyingi inaonekana kwamba jukumu la kusaka fedha linapaswa kuwa la wanaume na jukumu la kusimamia gharama za maisha ni la wanaume na wanawake kwa pamoja.
News ID: 452

Nasaha ya Uislamu kwa Anayetaka Kuoa (sehemu ya 2)

3. Ukomavu wa kiuchumi

Ukomavu wa kiuchumi inamaanisha kuwa na uwezo na ujuzi wa kutafuta pesa, kuhifadhi pesa hizo, usimamizi mzuri wa pesa hizo na uendeshaji mzuri wa gharama za maisha. Katika baadhi za tamaduni, mara nyingi inaonekana kwamba jukumu la kusaka fedha linapaswa kuwa la wanaume na jukumu la kusimamia gharama za maisha ni la wanaume na wanawake kwa pamoja. Lakini katika tamaduni zetu za kiafrika, jukumu la kusaka fedha ni jukumu la wanandoa kwa pamoja na iwapo jukumu hili litabebwa na mmoja wao, basi mshirika wa pili ataonekana kuwa ni mzigo. Mbaya zaidi ni kupata mwanaume ambaye ameacha jukumu hili kwa mke wake. Kwa ibara za kisasa, mme huyu analelewa na mke wake. Hii ni aibu kubwa kwa mwanaume na limekemewa mno katika tamaduni yetu ya kiafrika na dini yetu tukufu. Hata hivyo, ieleweke kuwa jukumu hili ni wajibu wa mwanaume na mwanamke ana hiari katika hili jambo. Min ghairi ya hayo, mwanamke lazima achukue ruhusa ya mme wake ili atoke nyumbani akafanye kazi.

Ishara za ukomavu wa kifedha kwa mtu

- Kufanya kazi katika kazi thabiti kwa angalau mwaka mmoja.

- Mshahara wa mtu uko katika kiwango kinachofaa kulingana na mapato ya wastani ya jamii na kazi yake ni ya wakati wote.

- Ana ujuzi wa kufanya kazi na hatimaye kupata pesa. Hii ina maana kwamba ikiwa atapoteza kazi yake ya sasa kwa sababu yoyote, bado anaweza kuajiriwa katika kazi sawa kulingana na ujuzi wake.

Je ukomavu huu unachunguzwa tu kwa mvulana anayetaka kuoa au hata kwa binti? Ukweli ni kwamba ukomavu huu unahusu watu wawili katika ndoa. Ukiwa binti unayepanga kuolewa, unahitaji ukomavu huu ili uweze kupanga na kusimamia ununuzi wa vitu na mahitaji mbalimbali ya maisha na kununua kila kitu kwa usahihi na kwa kiasi kinachohitajika kulingana na ratiba. Ikiwa utajikuta katika hali ambayo maisha yako yanakabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha, lazima uweze kusimamia gharama za kila siku za maisha vizuri katika hali hii pia. Ikiwa wewe ni mwanamke unayefanya kazi pamoja na mumeo na kupata pesa, ukomavu wako katika hili sekta itadhihirika hapa. Ieleweke kuwa mvulana anayetaka kuoa ni lazima awe na kazi na awe amefanya kazi kwa muda wa angalau mwaka na kuwekeza na kujipanga kunako kuoa. Sio busara kupata kazi leo, kisha baada ya mwezi ukataka kuoa. Kwa upande wa binti, sio sharti kuwa awe na kazi pindi anapotaka kuolewa. Yumkini akapata kazi baadae katika maisha yake ndani ya ndoa. Lakini kwa mvulana, ni kosa la jinai kuoa bila kuwa na kazi au chanzo cha mapato. Kwa hiyo, ushauri kwa mvulana anayetaka kuoa ni sharti kwamba awe na kazi na awe ni mchapakazi na mtu mwenye bidii ya kuchakarika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia yake.

4. Chunguza sifa zake kuu

Je mtu huyu anayetaka ushauri ni mtu mwenye sifa zipi kuu? Je ni mtu mpole au mshari? Mwenye bidii au mzembe? Ni mtu wa dini au la? Ni mwenye kuheshimu watu au ni mtu mwenye tabia mbaya? Ni muaminifu au la? Ni mkweli au muongo? Ni mtu mwepesi wa kufanya mambo au ni wa kujivuta? Ni mtu mwenye kujituma au lazima asimamiwe katika kazi zake? Ni mwenye subira au ni mwepesi wa kupandwa na mori? Ni mvumilivu au la? Hizi ni baadhi za sifa ambazo zinabainisha hulka na maumbile ya mtu kwa ujumla. Kama mtoaji wa shauri, unapaswa kujua sifa kuu za msemezwa wako ili ujue anafaa kuoa au kuolewa na mtu mwenye sifa zipi. Kwa mfano, kama mwanaume ni mtu mwenye hasira za mkizi, basi hapaswi kuoa mwanamke mwenye hasira kama yeye. Badala ya kuwa na bwana harusi na bi harusi katika ndoa hii, tutakuwa na bwana moto na bi moto! Ugomvi, vita na hata mauaji yatapatikana katika ndoa hii. Mtu wa hasira za mkizi anapaswa kuoa mwanamke mwenye subira na sio mwenye kidomodomo maana waswahili husema mdomo uliponza mwili!

Vile vile, mtu wa dini anapaswa kuoa mtu wa dini pia, la sivyo, hapatakalika humo nyumbani. Mtu mzembe akioa mzembe mwenzake, maisha yao hayatakuwa na maendeleo yoyote kwani wote wawili wanahitaji kusukumwa na hakuna mwenye kusukuma mwenzake hapa. Lakini mzembe akiolewa na mtu mchapakazi na mwenye kujituma, basi huyu mzembe atarekebika hatua kwa hatua.

Katika kuchunguza sifa zake, ni muhimu pia kujua yeye msemezwa binafsi anapendelea mwanandoa mwenzakea awe na sifa zipi. Kama ni mwanaume, je, anataka mwanamke mpole au asiye mpole? Anataka mwanamke aliyesoma hadi ngazi za juu au ambaye hajasoma sana? Anataka mwanamke wa kujiheshimu au la? Anataka mwanamke bora au bora mwanamke? Haya yote ni mambo ya kuzingatiwa kabla hujatoa ushauri wako maana kumbuka lengo la ushauri ni kuzaa matunda mazuri.

5. Chunguza mazingira ya sehemu anayoishi

Kama kuna kitu huwa kinaathiri maisha ya mwanadamu, ni mazingira anayoishi. Hapa kama mshauri, lengo letu ni kujua sehemu anayoishi msemezwa na sifa kuu za watu wa eneo hilo. Kwa mfano mtu huyu akisema kuwa anaishi sehemu ambayo inasifika kwa kilimo, bila shaka utang’amua kuwa mtu huyu ameathiriwa na bidii, kujituma na subira ya wakulima kutoka eneo lake. Akisema anatoka sehemu ambapo inasifika kwa biashara, basi kama mshauri, utajua fika kuwa huyu mtu ni mtafutaji kutokana na athari ya kuishi na watu wapambanaji katika maisha yake.

Katika mazingira ya maisha ya kiafrika, hapa pia tutaangazia umuhimu wa kabila la msemezwa. Sisi wenyewe kwa wenyewe tunajuana kwamba kila kabila lina sifa lake kuu. Kwa mfano ukija Kenya, sifa kuu ya Wakikuyu ni watu wenye uchu wa kusaka hela kwa udi na uvumba. Sio watu waliobweteka, bali, ni watu wachakarikaji katika maisha yao na hata maendeleo walionayo ni ushahidi tosha kunako hili. Ukija Tanzania, Wachagga ndio wanamiliki sifa hii. Ukienda Nigeria, Waigbo ndio wenye sifa hii na ukienda Ghana, Waashanti ndio wenye sifa hii.

Ukidurusu makabila haya yote yanayoongoza katika utajiri katika nchi hizi mbalimbali, utagundua kuwa, kutokana na akili zao za kifedha na uwezo wa kuvutia wa kifedha, makabila haya yamevuka changamoto za asili yao na kuibuka kuwa makabila ya utajiri zaidi barani Afrika. Kwa mujibu wa haya tuliyosema, akija mmoja kutoka kwenye haya makabila tuliyotaja, bila shaka, kama mshauri, utakuwa na picha kamili kumhusu na utajua anafaa kuoa au kuolewa na mtu yupi na mwenye sifa zipi. Ndio, sio lazima aoe mtu wa kabila lake, lakini ni lazima aoe mtu ambaye sifa zake zitaendana kutokana na mazingira ya sehemu anayoishi.

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: