Surat Falaq
(asubuhi)
Ina aya 5 na imeteremshwa Makka
Mambo yaliyokusanywa na sura hii
Sura hii nayo ni kama ambavyo
tuliona katika surat Nass, kwamba ni sura ambazo ziliteremshwa kwa Mtume (saww)
kwa lengo la kumpa mafundisho yeye na umma wake jinsi ya kujikinga kwa Mwenyezi
Mungu kutokana na shari za ulimwengu huu, hivyo basi sura hii pia inaingia
katika mfumo wa sura ambazo ni kinga.
Na sura yenyewe ni kama ifuatavyo:
بِسْمِ
اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
"Kwa jina la Mwenyezi
Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu”
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ
الْفَلَقِ (1)
(1)
"Sema ewe Mtume kwamba
unajilinda kwa mola wa asubuhi”.
Neno "falaq” katika lugha ya Kiarabu
lina maana ya kuchambua na kutenganisha kitu, lakini tunaona hapa Mwenyezi
Mungu analitumia neno hili kwa kumaanisha asubuhi, hii ni kutokana kwamba
asubuhi kama tunavyojua kuwa ndio ambayo inapasua giza na kuweza kudhihiri,
hivyo basi ni maana ambazo zinaendana kwa karibu.
مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ (2)
(2)
"Unajilinda kutokana na shari ya alichokiumba”
Kwamba unaelekea
kwa mola wako kutokana na shari ya viumbe vyake, viwe ni watu au majini. Lakini
hii haina maana kwamba Mwenyezi Mungu ameumba mambo ambayo ni shari mpaka sisi
tuwe ni wenye kujikinga nayo kwake, hapa ni lazima kwanza tuelewe maana ya
kuumba kisha ndio tujue kwamba Mwenyezi Mungu hakuumba shari. Kuumba kama
inavyoelezewa kwamba ni kuleta kitu katika uwepo baada ya kuwa hakikuwepo, na
kwa maana hii bila shaka ni jambo la heri ila tu shari itakuja kwa kitu kile
baada ya kuwa kimeumbwa na kimechukua vipi nafasi yake katika utekelezaji. Kama
kitabakia katika asili yake basi kitaendelea kuwa heri, na kama kitatoka katika
mfumo sahihi basi kitakuwa shari.
وَمِنْ شَرِّ غَاسِقٍ
إِذَا وَقَبَ (3)
(3)
Na pia unajilinda na shari ya usiku mzito
unapoingia”
Na
hii ni kutokana kwamba viumbe wabaya mara nyingi sana wamekuwa wakitumia usiku
kama ngao ya kufanya mabaya yao. Hivyo basi unajikinga kwa Mwenyezi Mungu
kutokana na shari za hawa viumbe ambao huwa na tabia kama hizi.
وَمِنْ شَرِّ
النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ (4)
(4)
"Na pia
unajilinda na shari za wenye kupuliza katika mafundo”
Ni
nani ambao hupuliza katika mafundo?
Wafasiri
wengi wa Quran wameeleza kwamba maana halisi ya wenye kupuliza kwenye mafundo
ni wanawake ambao hufanya kazi za kuroga na uchawi. Lakini pia maana ya neno "wenye
kupuliza katika mafundo” inaweza kuwa pana zaidi ya kuishia tu kwa wachawi,
kwani hata ambao wanakuwa na nia ya kuchonganisha au umbea na kutenganisha
baina ya walioungana pia wanaingia katika maana ya neno hili, hivyo basi hakuna
kizuizi kama itakuwa kwamba tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kila
ambaye anakuwa na lengo baya kwetu.
وَمِنْ شَرِّ حَاسِدٍ
إِذَا حَسَدَ (5)
(5)
"Na pia unajilinda kuokana na shari ya hasidi
anapofanya husuda zake”
Katika
aya hii tunafahamu ya kwamba husuda ni katika sifa mbaya mno, na ndio maana
Mwenyezi Mungu ameiweka miongoni mwa mambo ambayo tunatakiwa tujikinge nayo.
Imepokelewa
riwaya kutoka kwa Imamu Sadiq as akisema " hakika husuda humaliza imani ya mja
kama ambavyo moto humaliza kuni ziwakazo”
Mwenyezi
Mungu atulinde na kila shari ambazo zinakuwa zinatuzunguka katika maisha yetu.
Sh
Abdul Razaq Rashid.