IMAMU MAHDI (as)
Katika ukurasa huu ningependa
kumzungumzia Imam wa zama hizi ambae ni maarufu kwa Jina la Imam Mahdi (a.s).
Pia ningependa kumzunguzia Baba yake pamoja na Mama yake kwa ujumla.
KUZALIWA KWAKE
Imam Mahdi (as) ni Imam wa kumi na
mbili wa Mashia, na Baba yake alikuwa anaitwa Imam Hassan Askarii(a.s). Imam
wetu Mutkufu alizaliwa katika siku ya Ijumaa Mwaka wa 255 katika Mji wa
Samar`ra na Jina la Imam Mahdi(a.s) ni kama Jina la Babu yake Mtume(s.a.w.w).
Wanahistoria wanasema; Jina hilo la hadharati
alipewa na Mtume Mtukufu (s.a.w.w) , kutokana na kufanana kwa Majina hayo ni
dalili tosha ya kwamba kudhihiri kwa Mtume ni kuwaondoa watu katika dimbwi la
ujinga, na kwa kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.s) ni kuwatoa watu katika giza
walilo kuwemo.
Lakabu za hadharati zimegawanyika
katika sehemu kuu zifuatazo:
Qaaim, Muntadhar, Hujjat, baqiatu
llah, Wali Asri, Swahiba Zaman na Mahdi. Haya Majina mawili ya mwisho ndio
Majina maarufu sana katika jamii.
Mama yake Imam Mahdi (as) alikuwa akiitwa Nargisi, wahakiki wamethibitisha
ya kwamba Mama huyo alikuwa ni Mtumwa.
KUZALIWA KWAKE KWA UFICHO
Imam Hassan Askarii (as) kipindi alipokuwa
kiongozi, watu wa Banii Abbasi walipatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na habari zilizotoka kwa Mtume (saw)
na Maimamu (as) kuhusu kuzaliwa Mtoto wa Imam Askarii (as), ambaye atakayekuja kuangamiza dhuluma, na kuweka Uadilifu. Imam
Askarii alikuwa akichunguzwa sana mpaka atakapozaliwa Mtoto huyo. Kutokana na
sababu hiyo kukawa kuzaliwa kwake ni kwa maficho na hakuna watu waliotambua
chochote kile kinachoendelea.
Imam Ridha(as) anasema: "moja
ya sifa ya Imam Mahdi ni kuzaliwa kwake
kwa maficho.” Na pia hadithi nyingi zinaeleza ya kwamba Imam anafanana
na Hadharat Ibrahim (as) na Hadharat Mussa(as).
ZAMA ALIZOISHI IMAM MAHDI
Zama alizoishi Imam zimegawanyika
katika sehemu kuu tatu; 1- Zama ya Ikhtifaa (maficho). 2- Zama ya Ghaibati
ndogo. 3- Zama ya Ghaibati kubwa.
1-Zama ya Ikhtifaa (maficho)
Hii zama ya Ikhtifaa (maficho) ni
wakati alipozaliwa Imam Mahdi(as) mpaka kifo cha Baba yake. Imam aliishi na
Baba yake kwa muda wa miaka(5) mitano, katika muda huo Imam Askari(as) alikuwa
na mamlaka makuu mawili, kwanza kumlinda Imam Mahdi(as) kutokana na maadui, na
la pili kumtangaza ni Imam wa kumi na mbili wa Mashia Duniani. Watu pekee wa
Nyumba ya Imam Askari(as) ndio walijua uzawa wa Imam huyo Mtukufu.
Baada ya muda Imam Askari(as)
aliwakusanya Mashia arubaini kwa ajili
ya kumtambulisha Imam Mahdi(as) ni Imam wa kumi na mbili baada yake. Baada ya
kuishi Samara pia alipelekwa Madina ambako huko aliishi na Babu yake kwa
maficho.
2-Ghaibatu Sughra (ndogo)
Baada ya kufariki Imam Askari(as)
katika mwaka wa 260 h.t ndipo ilianza
ghaibati ndogo ya Imam Mahdi(as), iliendelea ghaibati hiyo mpaka mwaka wa 329
hijiria kamaria. Katika kipindi cha ghaibati ya Imam(as) alikuwa akiwasiliana
na watu maalum, ambao hao watu walikuwa wakiwasilisha masuala mbalimbali ya
kidini kutoka kwa Imam mtukufu(as) watu hao ni miongoni mwa mashekhe wakubwa wa
Kishia, pia kazi nyingine kubwa waliokuwa nayo ni jinsi gani ya kuwaandaa watu
kwa kuipokea ghaibati kubwa ya Imam Mahdi(as)..
3-Ghaibati Kubra (kubwa)
Hiki ni kipindi kirefu cha kupotea
kwa Imam Mahdi(as), kipindi hiki kilianza baada ya kuisha kupotea kipindi
kifupi cha Ghaibati, kupotea kwake kurefu Imamu (as) kutaendelea kipindi hichi
mpaka hapo atakapo penda Mwenyezi Mungu kumdhihirisha Imam wake.
Katika muda huu ambao Imam hayupo, kuna Naibu wake anayeitwa
kwa jina la Walii Faqih, yeye ndiye anayesimamia masuala yote ya Dini,
Waislam wote kwa ujumla wanatakiwa
kumfuata na kumsikiliza katika kila jambo, mpaka hapo atakapo dhihiri Imam
Mahdi Mtukufu (as).
Imeandikwa na Dada Nuru Sudi.