bayyinaat

Published time: 06 ,April ,2017      16:53:09
Wataalamu wa maswala ya tamaduni wanajaribu kwanza kutuambia kuwa kuna aina mbili za sababu ambazo ndio chimbuko la kuanguka kwa tamaduni yoyote ile, nazo ni kama ifuatavyo:
News ID: 73

SABABU ZINAZOPELEKEA KUANGUKA KWA TAMADUNI

Baada ya kuelezea mtazamo sahihi juu ya sababu zinaopelekea kupatikana au kuzalika kwa tamaduni, sasa tuingie katika sehemu ya tatu ambapo tutajaribu pia kuzungumzia sababu zinazopelekea kuanguka kwa tamaduni hiyo, na hapa pia tutakuja na mitazamo mbalimbali katika kubainisha swala hilo.

Wataalamu wa maswala ya tamaduni wanajaribu kwanza kutuambia kuwa kuna aina mbili za sababu ambazo ndio chimbuko la kuanguka kwa tamaduni yoyote ile, nazo ni kama ifuatavyo:

Moja: sababu ambazo ni za ndani ya wahusika wa tamaduni, kwa maana ya kwamba sababu hizi huwa zinatokana au zinapatikana bila ya kuangalia sehemu ambayo tamaduni husika inapatikana, kwa maana nyengine bila ya kuangalia mazingira ambayo tamaduni ile inapatikana. Na sababu hizo ni kama:

1. Migogoro

2. Kutokubali kwamba asiyekuwa wewe anaweza kuwa na jambo bora nk.

Kwa hiyo tamaduni yoyote ambayo itakumbwa na mambo kama haya basi ni lazima itakuwa ni yenye kuanguka na kutodumu.

Mbili: sababu ambazo ni za nje, kwa maana ya kwamba sababu hizi ni lazima mazingira yanayopatika tamaduni husika pia yaweze kuhusika, kwa maana sasa zile vurugu na migogoro inatoka katika nafsi za wanadamu na kuhamia katika mazingira wanayoishi. Na sababu hizi ni kama:

Moja: matumizi mabaya ya mazingira

Mbili: matumizi mabaya ya maliasili

Hapa wataalamu hawa wanajaribu kutueleza kwamba endapo wanadamu watakuwa ni wenye kutumia vibaya au kuharibu mazingira wanayoishi, basi tamaduni yao pia itapotea, kwa sababu mazingira ni kipengele muhimu sana katika kuendeleza na kudumisha tamaduni yoyote ile. Hali kadhalika kuhusiana na maliasili pia.

Angalizo

Bado pia katika utafiti huu tunakutana na tatizo ambalo tulikutana nalo wakati tunazungumzia sababu ya kupatikana kwa tamaduni, nalo ni kwamba, watafiti hawa wamefikia katika kuelezea athari ambazo zinapatikana baada ya kuharibika kwa tamaduni, badala ya kuelezea sababu iliyopelekea kuharibika kwa tamaduni ile.

MTAZAMO SAHIHI WA QURAN

Kabla ya kubainisha mtazamo sahihi wa Quran katika swala la kuanguka na kupotea kwa tamaduni, ni lazima kwanza tuweze kutambua kwamba Mwenyezi Mungu (swt) hakuna hata wakati mmoja ambao anauangamiza umma ikiwa kwamba umma ule ulikuwa ni wenye kushikamana na mafundisho sahihi. Na pia ni lazima tutambue kwamba Mwenyezi Mungu siku zote ni mwenye kuwakumbusha waja wake kuhusiana na mfumo sahihi wa kuishi ili waweze kufikia katika kilele cha mafanikio na wasiweze kuangamia au kupotea. Na ndio maana unakuta katika Quran tukufu, sehemu nyingi sana ambazo Mwenyezi Mungu (swt) anatukumbusha kuhusiana na watu waliopita pamoja na kutuelezea mwisho wao ulikuwa vipi na ni sababu gani ilipelekea wao kuwa na mwisho kama ule. Mwenyezi Mungu anasema:

"لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ

"hakika katika visa vyao kuna mazingatio kwa wenye kuwa na akili (kufikiri) ”[1]

Kwa maana ya kwamba kila kisa ambacho kinaelezwa katika Quran basi kinakuwa na malengo na mafunzo yake pia, na si kwamba kinakuja tu bila ya kuwa na malengo. Na miongoni mwa malengo ambayo sisi leo hii tunanufaika nayo katika mada hii, ni kuweza kutambua sababu iliyopelekea kufaulu au kufeli kwa tamaduni katika zama zilizopita. Na hii ni kutokana kwamba kama ambavyo sisi leo hii tunaishi, basi hata wao pia walikuwa wakiishi, na kama ambavyo sisi leo hii tunajivuna kuwa na tamaduni basi hata wao pia walikuwa na tamaduni zao, lakini kutokana tu na sababu miongoni mwa sababu waliweza kuzipoteza tamaduni hizo.

Kwa hiyo kwa namna yoyote ile bado sisi ambao tunaishi sasa hivi tuna haja ya kuzisoma zama zilizopita na kisha kuweza kuchukua masomo katika hayo. Na ndio maana unakutana na sehemu nyingi mno katika Quran, kwamba Mwenyezi Mungu anaelezea visa vya watu wa aina mbalimbali na jinsi walivyokuwa wakiishi na jinsi gani waliweza kufikia tamati na je ulikuwa ni mwisho mzuri au la? Na kama ulikuwa mwisho mzuri basi nini sababu ya hilo, na kama pia ulikuwa mwisho mbaya basi ni ipi sababu yake pia.

Hebu angalia aya hii baada ya Mwenyezi Mungu kutaja na kuelezea kisa kizima cha nabii Mussa (as), alikuja na kusema :

إن في ذلك لعبرة لمن يخشى"

"kwa hakika katika hayo kuna mazingatio kwa wenye kuogopa[2]

Na pia sehemu nyengine anatukumbusha na kutuambia:

قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ

"kwa hakika kabla yenu kumepita aina nyingi mno za mienendo, basi tembeeni ardhini katika hali ya kuangalia ni jinsi gani ulikuwa mwisho wa wapingaji[3]

Kwa maana ya kwamba nyinyi sio viumbe wa kwanza kuishi katika ardhi hii, bali kuna ambao walikuwa kabla yenu, lakini cha msingi si kwamba walikuwa kabla yenu, bali ni namna gani walikuwa? Je walikuwa na mwisho mzuri au mbaya? Na je, nyinyi pia mnataka kuwa na mwisho kama ule mbaya au ule mzuri?, haya yote ni mambo ambayo tunakutana nayo pindi tunaposoma Quran tukufu, lakini ni aina gani ya mfumo ambao tunauchagua ni juu yetu sisi wenyewe, tena baada ya kujua kuwa mfumo huu unapelekea katika mwisho huu na mfumo ule unapelekea katika mwisho ule.

Sasa hii ni baadhi ya mifano tu ambayo tumeweza kuileta hapa ili kubainisha kwamba Quran inapoleta kisa cha watu waliopita basi inakuwa ndani yake kuna lengo na inatutaka sisi ambao tunaishi sasa tuweze kufahamu lengo hilo , ili yasije kutupata yale ambayo yamewapata waliopita kutokana na mfumo ambao wao waliuchagua, au tuweze kufikia katika yale ambayo wameyafikia ambao walichagua mfumo mzuri.

Na kutoka na kusoma visa vya watu waliopita na mifumo ya maisha yao kwa mujibu ambavyo Quran imetuelezea, sasa tunaweza moja kwa moja kutaja sababu ambazo zinapelekea kuanguka na kutoendelea kwa tamaduni yoyote ile, na hizi ambazo tutazitaja hapa ni sababu ambazo tunaweza kuzifahamu kutokana na Quran tukufu.



[1] Suratul yusuf aya 111

[2] Suratul naziat aya 26

[3] Suratul alimran aya 138

maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: