bayyinaat

Published time: 16 ,April ,2017      23:16:20
Akili inamfanya mtu awe na mwelekeo katika mambo yake yote anayoyafanya, na hasa mambo yanayohusu maisha yake ya kila siku na ya baadaye. Kwa hiyo basi.........
News ID: 76

Katika mtazamo wa Kiislamu, akili ni kitu bora sana, na vitu vingine vilivyobakia havikaribii ubora wake, ukiiachia mbali kulingana au kuwa sawasawa.

Na ubora huo umetokana na sababu nyingi, moja wapo ni hii:

Akili inamfanya mtu awe na mwelekeo katika mambo yake yote anayoyafanya, na hasa mambo yanayohusu maisha yake ya kila siku na ya baadaye. Kwa hiyo basi wakati wowote jamii au mtu wa kawaida anapokosa mwelekeo katika mambo yake na hasa maisha yake, inatosha peke yake kuwa dalili inayojulisha kutoweka akili yake katika uwanja wa maisha yake (yaani, kuinyima akili nafasi ya kutoa mwongozo na kuonyesha njia ya mafanikio katika mambo yake).

Na mimi nimechagua mada hii kwa sababu nimegundua kwamba kupoteza mwelekeo ni katika matatizo makubwa yanayoisumbua jamii yetu ya Kitanzania.

Akili ni nini?

Akili ni nguvu nyepesi inayojumuika pamoja na umbile la mwanadamu kama chombo kinachomuwezesha binadamu kudiriki baya na zuri, heri na shari, haki na batili na pia humuwezesha kufikiri na kujua uhakika wa vitu kuelewa hatima ya mambo kabla ya kutokea.

Ikiwa hiyo ndio maana ya akili ni kwa nini inapingana na hali halisi ya maisha ya watu wengi?

Tunaporejea maisha ya watu, tunakuta batili na shari, imetawala na kumiliki robo tatu nzima ya maisha yao, na haki au mema yamebakia kuwa ni historia isiopigiwa mfano katika maisha ya kijamii, na wakati fulani watu wengi wanafanya batili na huku wakidhani kuwa ni haki, jee hii ina maanisha kwamba Mungu katubadilisha kuwa viumbe wasio na akili, bila ya sisi kujijua na kubakiwa na wanadamu wenye akili ni wale wa karne zilizopita?

Jawabu: Majibu ya maswali hayo ni kama ifuatavyo:

Tunapaswa kujua kwamba akili ya mwanadamu pamoja na kuwa kwake muhimu lakini ina mipaka yake, kwa sababu kama hiyo utakapotaka kuinasibisha jambo lolote, upande wake kwanza kabisa, hakikisha jambo lako lisiwe nje ya mipaka hiyo. Moja katika mipaka ni;

1)Akili inamfanya mtu atofautishe mazuri na mabaya lakini haimlazimishi mtu kutenda.

Kwa hiyo tunapaswa kujua ni kitu gani ninachomsukuma mtu atende jambo au asitende? Na jawabu lake utakuwa ni ufumbuzi wa matatizo ya kitabia yaliyoashiriwa katika maswali ya awali.

2)Ndugu zangu, pembeni ya akili ya binadamu kuna kitu kinaitwa (imani) na Imani ndio inayotengeneza tabia ya mtu na mwenendo wake katika maisha, na halikadhalika jamii yeyote ulimwenguni, hujengwa kupitia msingi huo, na haijatokea wala haitatokea ulimwenguni jamii ya aina yoyote, inayoweza kuishi basi itikadi au imani inayopangilia nidhamu ya maisha ya jamii hiyo, kwa sababu kama hiyo basi tambua yafuatayo:

Imani, itikadi ndio inayomtambulisha mtu katika dunia hii, na ndio ambayo inayomuekea mtu mipaka katika namna ya kuhusiana kwake na mazingira pia na jamii yake iliyomzunguka.

Na hayo mahusiano yake na mazingira yake au jamii yake, ndio yanayotengeneza historia ya mtu, au historia ya umma ulimwenguni.

Na kwa kuwa historia (sawa ya mtu sawa ya jamii) ni kitu muhimu mno katika maisha, basi inatakikana imani au itikadi iwe na uwezo wa kuendesha mambo na harakati zote anazozifanya mwana adamu katika maisha yake. Na imani ili imuongoze mtu au jamii, ni lazima idhamini matarajio na malengo ya harakati za mtu yule maishani mwake.

Na ili (imani au itikadi) iweze kudhamini hayo, ni lazima yenyewe kama itikadi iwe na mafungamano na yale maisha halisi ya mwanadamu katika dunia hii.

Sasa ndugu msomaji ikiwa imani inatakiwa iwe katika mazingira kama hayo, ni nani, au jamii gani inayoweza kudai imani kama hiyo? Jawabu ni hakuna.

Na kukosekana na imani kama hiyo ndio sababu ya maovu, dhulma na ushenzi wote unaofanyika, na bila shaka imani hiyo si kitu kingine zaidi ya Uislamu, Uislamu ndio imani pekee ambayo haijamuwacha mwanadamu afanye anachotaka sawa liwe dogo au kubwa, bali kila anachotaka kufanya au kufikiria utakuta Uislamu tayari umekwishamuwekea misingi inayomlazimu mtu yule kuizingatia katika kuyakimbilia au kuyafanya mambo yake.

Sasa mwanadamu anapozingatia ile misingi ya Uislamu na kuifanyia kazi ndipo imani yake inazidi kukua na kuchanua kifuani mwake na kadri imani inavyozidi kupanuka na kukomaa, na akili inavyozidi kupanuka na imani pia inazidi kuboreka na kuongezeka, kwa hivyo basi falsafa kubwa ya kuumbwa akili ni ile ije ishirikiane na imani katika kumkamilisha mwanadamu. Na mwanadamu yeyote atakayeshindwa kuzingatia misingi ya Kiislamu basi itadhoofika imani yake na akili yake, na hiyo ndio sababu ya kukosa mwelekeo katika maisha yake, au kuwa dhalimu au kuwa mwovu au kuwa na maisha mabaya yasiyotamanika.


maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: