bayyinaat

Published time: 08 ,May ,2017      10:37:19
Ni jambo ambalo lipo wazi kwamba katika dini ya Uislamu kulikuwa na vita nyingi mno ambazo Waislamu wakishinda, lakini ushindi ambao Mwenyezi Mungu anamuahidi mtume wake hapa ni ushindi juu ya kuufungua mji wa Maka kutoka katika mikono ya waabudu masanamu, hasa ukiangalia kwamba Waarabu walikuwa hawaamini kwamba itatokea siku moja Maka ikawa katika mikono ya Waislamu, na kama itatokea ikawa hivyo basi bila shaka Mtume atakuwa ni wa kweli na haki, maana haiwezekani ambaye ni mwongo kuja kuikomboa....
News ID: 83

Tafsiri ya Surat Nasr

(Msaada wa Mwenyezi Mungu)

Imeteremka Madina na ina aya 3

Mambo yanayokusanywa na sura hii

Sura hii imeteremka katika mji mtukufu wa Madina baada ya kuwa mtume ameshahamia mji huo, ikiwa imekuja na bishara njema kwa Mtume kwamba ushindi utakuwa upande wake na watu wataingia katika dini ya Uislamu makundi kwa makundi, na pia ikimpa Mtume njia pekee ya kumshukuru mola wake ni kwa kuzidisha kumtaja na kumsifia.

Ni jambo ambalo lipo wazi kwamba katika dini ya Uislamu kulikuwa na vita nyingi mno ambazo Waislamu wakishinda, lakini ushindi ambao Mwenyezi Mungu anamuahidi mtume wake hapa ni ushindi juu ya kuufungua mji wa Maka kutoka katika mikono ya waabudu masanamu, hasa ukiangalia kwamba Waarabu walikuwa hawaamini kwamba itatokea siku moja Maka ikawa katika mikono ya Waislamu, na kama itatokea ikawa hivyo basi bila shaka Mtume atakuwa ni wa kweli na haki, maana haiwezekani ambaye ni mwongo kuja kuikomboa Maka kwani Mwenye nyumba tukufu hatomuacha na atamuangamiza kama ambavyo ilitokea kwa Abraha na jeshi lake la tembo. Hivyo swala la watu kuingia katika dini ya Uislamu makundi kwa makundi baada ya mtume kuikomboa Maka ni swala linalofuatia bila kuuliza, kwani watakuwa wameshajikinaisha kwamba Mtume ambaye ameikomboa ni Mtume wa kweli.

Miongoni mwa majina ya sura hii ni (Taudii) ikiwa na maana ya "kuaga”, na hii ni kutokana kwamba ushindi wa dini ya Kiislamu ni ishara tosha kabisa ya kwamba muda wa kuishi mtukufu Mtume umekwisha. Imepokelewa riwaya kwamba ilipoteremka sura hii, Mtume aliwasomea masahaba zake nao wakafurahi sana, lakini alipoisikia Abbas mjomba yake Mtume haikuwa hivyo kwani alilia sana, na alipoulizwa na Mtume juu ya kulia kwake akasema " hakika naona kabisa kwamba umeanza kujiombolezea ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu”.

Fadhila za kusoma sura hii

Imepokelewa kutoka kwa Imamu Sadiq (as) "mwenye kusoma sura hii katika sala zake za faradhi au suna basi Mwenyezi Mungu atampa ushindi dhidi ya maadui zake wote, na siku ya kiyama atafufuliwa akiwa na kitabu ambacho kitakuwa kinatamka heri na kumpa bishara njema ya kuepukana na moto wa jahanamu, na hatopitia kitu siku hiyo ila kitakuwa kinampa bishara njema mpaka atakaoingia peponi”.

Kama ilivyo kawaida kwamba malipo haya ni kwa mwenye kuisoma sura hii na akashikamana na ambayo Mtume alishikamana nayo.

Na sura yenyewe ni kama ifuatavyo:

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu

إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ وَالْفَتْحُ (1)

(1) Utakapokuja msaada wa Mwenyezi Mungu na ushindi.

وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ أَفْوَاجًا(2)

(2) Na ukawaona watu wanaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi.

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ ۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا (3)

(3) Mtakase mola wako na umsifu kwa sifa njema na umuombe msamaha, kwani yeye ni mwenye kusamehe mno.

Pindi yatakapotimia.....

sura hii imekuja kuashiria kunako mambo matatu ambayo ni:

1. Msaada wa Mwenyezi Mungu

2. Ukombozi au ushindi

3. Kuingia watu katika dini makundi kwa makundi

Na ukiangalia hata mpangilio wa mambo haya utakuta kwamba nukta ya msaada wa Mwenyezi Mungu imetangulia, hii ikiwa na maana kwamba ndiyo kuna haja ya wanadamu kuandaa mipango kwa ajili ya kutimiza lengo fulani, lakini mipango hiyo siyo kila kitu katika kutimia malengo yale, bali kunahitajika msaada wa Mwenyezi Mungu kwa kila namna. Na ni wachache mno ambao huamini kwamba msaada wa Mwenyezi Mungu ndio kila kitu katika kutimia tupangayo.

Pia ukiangalia katika mpangilio wa mambo hayo matatu utagundua kwamba yamekaa katika mfumo wa sababu na kinachosababishwa, kwa maana ya kwamba msaada wa Mwenyezi Mungu ni sababu ya Mtume kupata ushindi na ukombozi, kama ambavyo kupata ushindi na ukombozi ni sababu ya watu kuingia katika dini makundi kwa makundi.

Mwisho kabisa Mwenyezi Mungu anamfundisha mtume wake na Waislamu kwa ujumla kwamba baada ya kufikia malengo kusudiwa kuna haja ya kushukuru.

Mwisho wa surat Nasr.

LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: