bayyinaat

Published time: 09 ,May ,2017      12:45:06
Kwa maana hizo hapo juu tunafikia katika natija ya kwamba, neno familia kwa maana ya kwanza kabisa linakusanya kila ambaye ni katika ukoo wa mtu fulani na sio tu kuishia kwa mke na watoto. Hiyo ni maana ya familia katika matumizi ya Waarabu kutokana na lugha yao.......
News ID: 87

Maisha ya kifamilia

Kwa kuangalia kichwa cha habari tu tunaweza kupata mwongozo wa kwamba ni jambo gani ambalo tunataka kuliongelea katika sehemu hii, nayo ni kwamba lengo letu ni kutaka kuzungumzia maisha yanayohusu familia kwa ujumla. Ila tu kwa kuongezea ni kwamba lazima tuweze kutambua kwamba sisi tutazungumzia maisha hayo kwa kuangalia misingi ambayo inapaswa hiyo familia iishi nayo. Hivyo basi kabla ya kuanza kuiangalia familia yenyewe, itakuwa ni muhimu mno kwanza kuanza kuelezea familia ni nini, na je familia inapatikana vipi, ni mambo gani ambayo yanaijenga familia katika misingi iliyo bora kabisa na ambayo hata Mwenyezi Mungu pia anairidhia.

Familia ni nini?

Katika kuelezea maana ya familia nitajaribu kuja na rai za watu mbalimbali ambao wamejaribu kuielezea familia kutokana na mazingira yanayowazunguka, nikiwa na maana ya lugha husika. Kwani kama ilivyo wazi kwamba lugha na lugha nyengine katika kuweka maana ya neno basi hutofautiana.

Tuanze na lugha ya Kiarabu ambapo tunakutana na kauli mbalimbali katika jambo hilo, anasema Firuz abad "neno familia kwa maana ya kwanza basi lina maana ya ngao ambayo mtu hujikinga nayo.....”.[1]

Kama ambavyo pia Ibn Athir pia anaelezea kwa kusema " familia ni neno lenye kumaanisha ukoo na watu wa karibu wa mtu fulani, na hii ni kwa sababu kwamba hao ndio ambao mtu huyo huwatumia kama kinga yake...”.[2]

Kwa maana hizo hapo juu tunafikia katika natija ya kwamba, neno familia kwa maana ya kwanza kabisa linakusanya kila ambaye ni katika ukoo wa mtu fulani na sio tu kuishia kwa mke na watoto. Hiyo ni maana ya familia katika matumizi ya Waarabu kutokana na lugha yao.

Wataalamu wa maswala ya jamii

Ama kuhusiana na wataalamu wanaohusika na maswala ya jamii wao wana mtazamo tofauti na ambao tumeutanguliza hapo juu, japokuwa wao pia hawakubaliani kauli moja katika kuelezea maana halisi ya familia. Kwani tunakuta kuna ambao wanasema "familia ni neno lenye kumaanisha watu maalumu wenye kukutanishwa na mahusiano fulani tena yenye nguvu..........”[3]. na kwa mujibu wa rai hii ni kwamba familia itaishia tu kwa wana ndoa na wala haitakusanya wengine. Huu ni mtazamo wa baadhi ya hao wataalamu wa maswala ya jamii. Ama kuna wengine mfano Dk Mardock ambaye yeye anaelezea familia kwa maana kama hiyo ya waliopita, ila yeye ameipanua zaidi. Anasema katika maneno yake " familia ni mkusanyiko wenye kusifika na sifa ya kuishi pamoja, kusaidiana kiuchumi, kuwa pamoja katika jukumu la kuendeleza kizazi. Na kwa uchache kabisa ni kwamba mkusanyiko huu utakuwa unakusanya mke, mume, na angalau mtoto mmoja anayetokana nao.....”[4]

Na hapa tunakuta kuna namna fulani ambayo ameweza kutanua maana ya familia, kwamba hata watoto pia wanaingia katika familia. Na mtazamo huu ndio mtazamo ambao wataalamu wengi sana wa maswala ya jamii wamekubaliana nao.

Mtazamo wa Kiislamu

Uislamu katika kuamiliana na jambo hili haukuja na maana moja nakusema kwamba ndiyo maana ya familia na maana zingine si sahihi, bali kama ambavyo umetumia njia hii katika maswala mengi pia katika swala hili umetumia njia hiyohiyo. Njia yenyewe ni kwamba, kila jamii iangalie wanafasiri vipi neno familia, je ni kwa maana ya kwamba kila ambaye ana undugu na mtu, au ni mahususi tu kwa ambao wapo chini yako, au ni mke, mume na watoto wao?. Lakini ni lazima tutambue kwamba, kwa maana yeyote ambayo tutafasiri neno familia basi kuna haki zake na misingi yake ya kuweza kuamiliana nayo, kwani Uislamu haujaacha jambo bila ya kuliwekea misingi.

Uhusiano wa familia na jamii

Bila shaka hakuna jamii ambayo itaundwa bila ya kuwa na vitu muhimu katika kuunda jamii ile, na kama tunavyojua kuwa jamii inatokana na watu, lakini je unadhani watu hawa watatoka nje ya familia?. Kama hapana basi tunafikia katika natija ya kusema kwamba familia kama familia ni msingi na nguzo muhimu sana katika kutengeneza jamii yeyote. Na kwa maana hiyo basi, endapo familia za jamii fulani zitasifika na sifa nzuri basi jamii kwa ujumla itasifika na sifa nzuri, na kama familia za jamii ile zikasifika na sifa mbaya basi pia jamii kwa ujumla itasifika na sifa mbaya.

Mwanamke na mwanaume

Mwenyezi Mungu katika kubainisha hekima yake, na kwamba familia ni lazima ianzie wapi, aliweza kuumba aina hizi mbili za wanadamu (mwanamke & mwanaume), na si tu kuumba bali pia aliweza kufanya kwamba kila mmoja katika hao ni kiungo muhimu kwa mwingine, kwa maana ya kwamba ili kipatikane kitu kamili basi ni lazima watu hawa wawe pamoja. Kama ambavyo ametueleza katika Quran kwa kusema:

هُنَّ لِبَاسٌ لَكُمْ وَأَنْتُمْ لِبَاسٌ لَهُنَّ

"....wao (wake) ni vazi lenu, na nyinyi (wanaume) ni vazi lao”.[5]

Akiwa na maana ya kwamba, kama ambavyo vazi hutumika kwa ajili ya kusitiri mwili na kujikinga kutokana na baadhi ya mambo, basi vilevile mahusiano ya kisheria baina ya mwanaume na mwanamke pia yanachukua nafasi ya vazi, kwani nayo humkinga mwenye kuwa katika mahusiano yale kutokana na mikengeuko mbalimbali.

Kisha angalia jinsi gani Mwenyezi Mungu alivyofanya kwa uwezo wake kwamba kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume kimaumbile na bila ya kulazimishwa na yeyote kwamba anamuhitajia mwenzake, na hii ni kutokana na namna ambavyo Mwenyezi Mungu ameweka kitu baina yao, na kitu hicho hakiwezi kupatikana mpaka wawili hao watakapokuwa pamoja. Na kitu hicho si kingine bali ni "Mapenzi” na "Huruma”, kama alivyosema katika Quran tukufu:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

"Na miongoni mwa alama zake ni kwamba kutokana na nyinyi amewaumbia wenza wenu ili muweze kupata utulivu kwao, na pia akajaalia baina yenu mapenzi na huruma, hakika katika hayo kuna mazingatio kwa watu wenye kufikiri”[6]

Kama tutaichunguza aya hii basi kuna mambo ambayo bila shaka ni lazima tuweze kuyaelewa, mambo hayo ni kwamba Mwenyezi Mungu ameashiria kunako nukta tatu muhimu sana katika msingi wa maisha ya kifamilia, na ambazo ni lazima zipatikane kwa mweza wako ili msingi wenu uwe ni madhubuti nukta hizo ni kama ifuatavyo:

1. Utulivu wa nafsi

Ikiwa na maana ya kwamba katika kila nafsi ya mmoja kati ya mwanamke na mwanaume kunakuwa na hali ya kutotulia, tunaweza kukataa jambo hili kwa midomo yetu na hata kwa vitendo vyetu, lakini uhalisia ndio huo kwamba pindi ambapo mwanaume au mwanamke anapokuwa peke yake basi na hata hali yake ya kiutulivu pia hupungua au isiwepo kabisa. Sasa ili hali hiyo ipatikane ni lazima wawili hawa waweze kuwa pamoja.

2. Amani

Kwa maana ya kwamba aya imeashiria kwamba Mwenyezi Mungu ameumba mke kutokana na nafsi ya mume, yaani ni kwamba mwanamke ameumbwa katika jinsi na aina ambayo inafanana na mwanaume kimaumbile, kwakuwa mwanaume ni mwanadamu na ameumbwa kwa udongo basi mwanamke pia amefanywa kuwa ni mwanadamu, kwa ibara fupi tunasema kwamba kuna usawa katika maumbile yao ili tu waweze kuwa pamoja.

Sasa unapopatikana usawa wa kuweza kukaa pamoja swala la amani linakuwa ni swala la kawaida baina yao, kwani hakuna ambaye jinsi yake ni ya mnyama mkali ili itokee kwamba anataka kumdhuru mwenzake.

3. Mapenzi na huruma

Ikiwa ni matunda yatokanayo na kupatana kwao katika maumbile, tabia, na hata mitazamo. Na ieleweke kwamba nukta hii ndio msingi mkubwa sana katika maisha ya kifamilia ambayo tunakusudia kuyaanzisha, kwani endapo hakutakuwa na mapenzi wala huruma baina ya waasisi wa familia basi familia hiyo itakuwa haina msingi thabiti.

Usikose kuungana nami katika wakati ujao ambapo tutakuwa tunazungumzia aina za familia.

Sh Abdul Razaq Rashid.



[1] Rejea Alqaamus

[2] Rejea Al nihaya

[3] Rejea Almujtamaa juz 2 uk 457

[4] Rejea Tabiatul mujtamail basharii uk 111

[5] Surat Baqara aya 187

[6] Surat Ruum aya 21

LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: