bayyinaat

Published time: 09 ,May ,2017      12:57:16
Wataalamu wa maswala ya kijamii wanatuambia kwamba katika jamii huwezi kukuta kwamba familia zote zipo katika mfumo mmoja, ikiwa na maana kwamba unaweza kuta familia hii na ile zinatofautiana kimfumo na hata kimalengo pia. Na aina au vigawanyo hivi vinatokana na........
News ID: 88

Karibu tena ndugu msomaji wa makala hizi katika sehemu na wasaa mwingine, wasaa ambapo utatupa fursa ya kuweza kutambua aina za familia katika jamii zetu na pia kuweza kutambua ni aina ipi ambayo inaweza kujenga familia yetu katika maadili bora kabisa.

Wataalamu wa maswala ya kijamii wanatuambia kwamba katika jamii huwezi kukuta kwamba familia zote zipo katika mfumo mmoja, ikiwa na maana kwamba unaweza kuta familia hii na ile zinatofautiana kimfumo na hata kimalengo pia. Na aina au vigawanyo hivi vinatokana na namna au jinsi gani familia husika inaamiliana na mtoto kimalezi, kwani muamala wao huu ndio unaweza kutuonyesha kwamba wao ni familia ya aina gani. Na vigawanyo hivi ni kama ifuatavyo:

1. Familia yenye chuki

Kwa maana ya kwamba mtoto katika familia hii huwa hapati mapenzi ambayo anastahiki kuyapata, na mwisho wa siku anakuwa ni mwenye kuchukiwa ima na baba au mama au hata wote wawili, na chuki inaweza kuwa inatokana na sababu ambazo wakati mwingine ni mambo ya wazazi wao wenyewe, lakini mwisho wa siku unakuta kwamba athari za matatizo yao hayo zinaangukia kwa mtoto. Basi unakuta mtoto huyu siku zote hana raha, amani, na wakati mwingine anatamani hata kwanini amezaliwa katika familia ile, kwa sababu anakosa hata uhuru wa kujieleza na kutoa mawazo yake. Welbery anasema katika kitabu chake "hakika chuki inaweza kubadili kabisa mfumo wa maisha ya mtoto na kumuweka katika mfumo mwingine, kwani humnyima amani na hata kuvunja hali ya kujiamini kwake, na mwisho wa siku mtoto huyu anaangukia katika mambo kama kuwa na moyo mgumu, wizi, kuwa na hamu ya kufanya makosa muda wote”.

2. Familia pokezi

Kwa maana ya kwamba familia hii ni familia ambayo inakubali kupokea nadharia na mawazo kutoka kwa mtoto wao, pamoja na hayo pia unakuta familia hii bado inaamiliana na mtoto wao muamala wa mapenzi na huruma. Na siku zote mtoto ambaye anapatikana na kukulia katika familia hii huwa ni mtoto bora na mwenye kuleleka vizuri, kwasababu hupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wazazi wake.

Mwana saikolojia Saimond anasema ".....wanajamii wema, watu wenye elimu, wafanyakazi bora, na hata wake wema hupatikana katika familia ambazo hupokea mawazo ya watoto na kuwapa mapenzi na huruma....”

3. Familia ya kibabe na kitemi

Kwa maana kwamba mtoto katika familia hii anakuwa ni mwenye kusikiliza na kutii tu yale ambayo wazazi wake wanayataka, na yeye kama yeye anakuwa hana nafasi ya kutoa mawazo wake. Jambo la muhimu ni kwamba katika familia hii inawezekana mtoto akawa ni mwenye tabia njema kutokana na tabia njema za wazazi wake, lakini bado kuna kasoro ambazo zitapatikana kwa mtoto huyu, ambazo ni:

1. Kukosa hali ya kujiamini na kujisimamia

Ndio, kwa sababu mambo yake yote yeye yamejengeka katika hali ya kubebewa mawazo na hata njia za ufanyaji, sasa itakapofikia wakati kwamba ni lazima afanye yeye kama yeye bila shaka hatokuwa na hali ya uthubutu, n ahata kama akithubutu kufanya bado hatokuwa na hali ya kujiamini kwamba anaweza.

2. Kujihisi kwamba ana mapungufu

Na hii ni hali ambayo inajijenga kinafsi, kwamba kwanini yeye kama yeye asiwe na nafasi ya kuzalisha mawazo au njia kadhaa za kuzalisha?.

3. Huwa ni mwepesi mno wa kuhadaika na kudanganyika na marafiki wabaya

Kwa sababu hawa marafiki pia huwa na njia za kuweza kumuhadaa mtu, sasa ikiwa mtoto hajalelewa katika malezi ya kuhoji na kutoa yake, bali ni katika malezi ya kukubali kila aambiwacho, bila shaka na haya ya marafiki pia atayakubali.

4. Familia ya demokrasia

Hii ni familia ambayo inakuwa inaendeshwa kidemokrasia kuanzia kwa wazazi mpaka kwa mtoto. Kwa maana ya kwamba mtoto katika familia hii huandaliwa kuwa mwanajamii kamili na ambaye ataweza kuishi na jamii inayomzunguka.

Ni ipi familia bora?

baada ya kuangalia vigawanyo hivyo vya familia, bila shaka tutakuwa tunajiuliza je, katika hizo ni ipi familia ambayo ni bora?. Katika kujibu swala hili ni lazima kwanza tuweze kurejea kila kipengele na kuona athari zinazopatikana, na bila shaka familia namba 1 na namba 3 haziwezi kuwa ni familia bora, kwa sababu hakuna ambaye yupo radhi kuona mtoto wake anaangamia katika madhara ambao yametajwa. Hivyo tunabakiwa na namba 2 na 4.

Na katika kujua familia bora kati ya hizo mbili ningependa kuashiria jambo moja ambalo ni swala zima la lengo, maana tukiangalia namba 2 tunakuta kwamba lengo la familia hili ni kumjenga mtoto wao katika msingi wa kuwa mwenye elimu bora, mchapakazi bora nk. Ila tukirejea namba 4 tunakuta kwamba lengo la familia hii ni kuweza kumlea mtoto katika malezi ya kuwa mwanajamii mzuri, bila shaka mpaka atakapokuwa mwanajamii mzuri basi bila shaka atakuwa amesifika na sifa nyingi mno nzuri. Ikiwa na maana kwamba hatakuwa na faida katika jamii endapo atakuwa ni mwenye elimu au mchapakazi mzuri, lakini maisha yake ya kijamii ni mabovu, na ikumbukwe kwamba lengo letu ambalo tunaanza nalo katika kujenge familia ni kujenga jamii. Kwa msingi huu ndio maana maulama wengi wamesema kwamba familia namba 4 ndiyo familia bora kabisa, kutokana na ukubwa wa lengo lake.

Familia na mwenendo wa mtoto

Lazima ifahamike kwamba familia ina mchango mkubwa mno katika swala zima la mwenendo wa mtoto, kama itakuwa ni familia njema basi mtoto pia atakuwa na mwenendo mzuri, na kama itakuwa ni familia yenye mienendo mibaya halikadhalika mtoto ataathirika na hilo.

Hivyo ni lazima tutambue kwamba mambo ya kiitikadi, dini, namna ya utendaji wa mambo mtoto hujifunza kutoka kwa familia yake.

Kuilinda familia

Miongoni mwa mambo ya muhimu mno kwa kila mwana familia ni swala zima la ulinzi wa familia ile, awe baba au mama, ni lazima ahisi kwamvba ana jukumu la kuilinda familia yake kutokana na kila aina ya uchafuzi wa kimaadili, kiitikadi, kidini na hata kijamii kwa ujumla.

Ungana nami katika wakati ujao ili tuweze kuangalia mambo ambayo yanapingana na familia katika misingi mpaka malengo.

Sh Abdul Razaq Bilal.

LABEL:
maoni Viewers
Name:
Email:
* Opinion: